Uongozi wa Wilaya ya Ruangwa na kamati ya ujenzi wapongezwa kwa kusimamia ujenzi wa majengo ya kituo cha afya.
Uongozi wa wilaya Ruangwa na kamati inayosimamia ujenzi wa majengo katika kituo cha afya Nkowe wamepongezwa na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kazi nzuri ya kusimamia ubora wa ujenzi wa majengo hayo.
Mhe. Majaliwa alitoa pongezi hizo wakati alipotembelea kituo cha afya Nkowe kukagua hatua ya ujenzi iliyofikiwa. Ambapo mpaka wakati anatembelea alikuta majengo yanayojengwa yakiwa katika hatua tofauti za umaliziaji na moja likiwa katika hatua ya lenta.
“Nimetembelea majengo yote yanayojengwa na kuridhishwa na kazi ambayo inafanyika, niwapongeze viongozi na kamati ya ujenzi kwa kazi nzuri ya usimamizi inayofanyika tena kwa kutumia mafundi wetu wa ndani. Kikubwa niwasihi muendelee kusimamia kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya ujenzi huu zinatumika vizuri na majengo yanajengwa kwa ubora unaotakiwa”, alisema Mhe. Majaliwa.
Aidha, Mhe. Majaliwa aliwataka watumishi wa afya kufanya kazi kwa kuzingatia maadili yao ya kazi na kwamba serikali inaendelea kuzifanyia kazi changamoto walizonazo. Pia alimuagiza Mganga Mkuu wa Wilaya kuhakikisha dawa zinapatikana moda wote katika kituo. Vilevile aliwasihi wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano kwa kushiriki katika shughuli za maendeleo katika maeneo yao zikiwemo za ujenzi wa miundombinu.
Kituo cha afya Nkowe kimenufaika kwa kupata ruzuku kutoka serikali kuu kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ili kuimarisha huduma za uzazi na mtoto ambapo kilipokea shilingi 500,000,000. Fedha hizo ndizo zinazotumika katika ujenzi wa jengo la upasuaji, ujenzi wa nyumba ya mganga, ujenzi wa jengo la maabara, ujenzi wa wodi ya mama na mtoto, ujenzi wa kichomea taka, ujenzi wa jengo la uzazi, ujenzi wa visima viwili vya kuvunia maji ya mvua na ujenzi wa choo cha matundu manne.
Mpaka wakati Mhe. Mjaliwa alipotembelea fedha kiasi cha shilingi 232,473,050 ndizo ziizokuwa zimetumika kwa shughuli za ujenzi. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ruangwa, Ndg. Adrea Chezue alimuhakikishia Waziri Mkuu kuwa vifaa vyote vinavyohitajika baada ya ujenzi wa miundombinu kukamilika vipo hivyo wanachosubiri ni majengo kukamilika ili vifungwe.
Katika mkoa wa Lindi miradi hii inatekelezwa kwenye kituo cha afya Nyangamara (Halmashauri ya Lindi) ambapo tayari shilingi 384,316,500 na Kituo cha afya cha Kilwa Masoko (Wilaya ya Kilwa)ambapo tayari shilingi 270,000,000 zimeshatumika. Vituo hivi navyo vilipokea shilling 500,000,000 kila kimoja na kazi za ujenzi zinaendelea ambapo majengo yapo katika hatua mbalimbali za umaliziaji.
Miradi hii itakapokamilika wananchi watanufaika kwa kupata huduma hizi muhimu karibu na maeneo yao tofauti na awali ambapo walikuwa wanalazimika kwenda umbali mrefu ili kupata huduma hizi.
Mhe. Majaliwa akitoa maelekezo baada ya kukagua
ujenzi unaoendelea katika kituo cha afya Nkowe.
Jengo jipya la upasuaji katika Kituo cha Afya Nkowe
Nyumba mpya ya mganga katika Kituo cha Afya Nkowe
Kichomea taka kinachojengwa katika Kituo cha Afya Nkowe
Jengo la zamani la kuhifadhia maiti
Jengo jipya la kuhifadhia maiti
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.