Wakulima na wajasiriamali Mkoani Lindi wameiomba serikali kuwasaidia mikopo kwa mtu mmoja mmoja ili kupima uwezo wao katika uzalishaji kwani ugawaji wa fedha kupitia vikundi umekua na changamoto nyingi zinazosababisha wengi wao kushindwa kukua kiuchumi .
Hayo yamesemwa katika ufunguzi wa Maonyesho ya Nanenane kwa Kanda ya kusini yaliyofanyika katika viwanja vya Ngongo, Mkoa wa Lindi ambapo mgeni rasmi alikua ni mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Ndg. Dustan Kyobya, Mkuu wa wilaya ya Mtwara.
“Serikali tunaiomba ingefikiria kutoka mikopo kwa mtu mmoja, kwenye vikundi wengi tunarudishana nyuma kwasababu sio kila mtu anakua na elimu na utayari wa kufanya ujasiriamali hivyo pesa tunayopata yeye anakua anatumia kwenye mambo yake mengine mwisho anashindwa kurejesha sehemu ya mkopo wake unakua mzigo wa kikundi kizima mulipe ili mpate mkopo mwingine’’ amesema Mjasiriamali kutoka wilaya ya Kilwa, Lindi.
Aidha, katika maadhimisho hayo, Mkuu wa wilaya ya Mtwara amewashauri wakulima kufanya kilimo biashara kwa kuongeza thamani ya mazao wanayoyazalisha kwa njia kama za usindikaji ili kuweza kuendana na soko shindani na kuongeza kipato chao binafsi.
Vilevile, ndg. Kyobya amelitaka Jeshi la magereza kuongeza uzalishaji na ufugaji wa Ng’ombe kwa ajiri ya nyama na maziwa na kubainisha fursa mbalimbali zilizopo kutokana na ufugaji huo.
“Mikoa ya Lindi na Mtwara kuna uhaba wa wafugaji wa Ng’ombe na hivyo kupelekea uhaba wa mazao hayo ya ufugaji hivyo suala la unywaji wa maziwa na ulaji sahihi wa nyama kuwa chini, lakini pia ufugaji huu utatupatia fursa nyingine ya kibiashara kwa kupata soko katika visiwa vya Comoro.”
Maonyesho ya Nanenane mwaka 2022 yanaenda kwa kaulimbiu isemayo “Agenda 10/30: Kilimo ni biashara, shiriki kuhesabiwa kwa mipango bora ya kilimo, mifugo na uvuvi.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.