Viongozi na watendaji watakiwa kutokuwa kikwazo kwa wawekezaji
Viongozi na watendaji mkoani Lindi watakiwa kutokuwa vikwazo kwa wawekezaji pale wanapotaka kuwekeza.
Haya yamesemwa na mkuu wa mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanywa ambaye alikuwa ni mgeni rasmi kwenye hafla ya uzinduzi wa kitabu cha mwongozo wa uwekezaji mkoa wa Lindi iliyofanyika katika ukumbi wa sea view beach resort – manispaa ya Lindi.
Byakanwa amesema kumekuwepo na tatizo la baadhi ya viongozi na watendaji kuwakwamisha wawekezaji pale wanapojitokeza kuwekeza katika mkoa, hivyo kuwafanya wakate tama huku wengine wakiamua kwenda kuwekeza katika maeneo mengine.
“Ni lazima viongozi na watendaji kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi pale wawekezaji wanapokuja kuwekeza katika maeneo yenu na sio kuwa moja ya vikwazo vya kukwamisha wawekezaji,” alisema Byakanwa.
Aidha, Byakanwa amewashauri viongozi wa mkoa na wilaya kuwaondoa wawekezaji feki ambao kazi ya ni kuchukua maeneo na kuyahodhi kwa miaka mingi bila kufanya chochote. Wawekezaji kama hao ni vema wakaondolewa na maeneo hayo wakapatiwa watu ambao wana nia ya kweli ya kuwekeza.
Mkuu wa mkoa Byakanwa amezitaka halmashauri kuzipitia upya tozo na ushuru ambazo zimeonekana kuwa kikwazo kwa wafanyabiashara na wawekezaji ili kuviondoa. Vilevile ameushauri uongozi wa mkoa kuendelea kusimamia maboresho yanayoendelea kufanyika katika miondombinu ya barabara, afya, elimu, kilimo n.k. kwa kuwa uimara wake unasaidia sana katika kuhamasisha uwekezaji.
Pia amewashauri viongozi wa mkoa kuhakikisha wanafanya vikao vya tathmini ambavyo watakuwa wakiwashirikisha wawekezaji na wafanyabiashara ambapo pia watajadili changamoto mbalimbali zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja.
Aidha, Byakanwa ameishauri TAMISEMI kuangalia katika muundo wa sekretarieti za mikoa na ile ya halmashauri kuwepo na maafisa Utalii na Viwanda ambao watasaidia kusimamia shughuli hizo katika ngazi husika. Kwani kwa sasa kumekuwepo na umbwe la kada hizo katika ngazi husika.
Mkuu wa mkoa Byakanwa pia ameusihi uongozi wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania kuanzisha bucha za nyamapori kama walivyoahidi kwani watanzania wanahitaji kula nyamapori.
Byakanwa alisema katika kuhamasisha utalii sio lazima kutegemea watalii kutoka nje bali wanaweza kuandaa siku ya kula nyama pori ambayo ingeweza kuandaliwa Kilwa Kisiwani ambapo watu watapata fursa ya kula nyama huku wakijifunza habari za magofu ya kale.
Lakini pia kupitia magofu unaweza andaliwa utalii wa usanifu wa majengo ambapo wataalam watapata fursa ya kwenda kujifunza namna majengo ya zamani yalikuwa yakijengwa ambayo mpaka sasa yapo imara tofauti na majengo ya sasa.
Byakanwa aliupongeza uongozi wa mkoa kwa kufanikisha kuandaa mwongozo kwa kushirikiana na taasisi ya ESRF na UNDP na kuweza kuuzindua. Pia aliwapongeza wadhamini waliofanikisha uzinduzi huo ambao ni UNDP, TAWA, Mashujaa FM na Lindi JUMBO.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema kuwa mkoa ulishafanya kongamano la fursa za kibiashara na uwekezaji ambapo moja ya azimio la kikao hicho lilikuwa ni mkoa kuandaa mwongozo wa uwekezaji. Hivyo uzinduzi wa mwongozo huo ni utekelezaji wa azimio hilo.
Zambi amesema licha ya kitabu cha mwongozo kubainisha maeneo yenye fursa za kibiashara na uwekezaji, pia kimeainisha maeneo ya kipaumbele katika uwekezaji kwenye mkoa. Maeneo ya kipaumbele ni pamoja na uwekezaji katika usindikaji wa mazao, uvuvi na ufugaji wa samaki, viwanda vya vifaa vya ujenzi, uchimbaji na uchakataji wa madini, kilimo cha umwagiliaji na maeneo mengine.
Pia wapo wawekezaji ambao tayari wameonyesha nia ya kuwekeza katika mkoa wa Lindi huku wengine wakiwa tayari wameshajenga viwanda na kuchukua maeneo kwa ajili ya uwekezaji.
Katika uzinduzi huo walishiriki wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, wawekezaji, wakuu wa taasisi mbalimbali, viongozi na watendaji. Pia mada mbalimbali ziliwasilishwa zikiwemo za TAWA, EQUINOR, SHELL, na nyingine.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.