Viongozi Tume ya Utumishi wa Umma wazungumza na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma Mkoani Lindi.
Viongozi wa Tume ya Utumishi wa Umma wamefanya ziara Mkoani Lindi kwa lengo la kukutana na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma na watumishi wa umma ili kuwaelezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Tume ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha kuhusu sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Akizungumza na viongozi wa taasisi za umma, Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bi. Salome Mollel alieleza kuwa tume ilianza kufanya kazi rasmi tarehe 7 January, 2004 ikiwa na kazi ya kufuatilia na kusimami uendeshaji wa shughuli za Rasilimali watu katika taasisi umma na kuhakikisha kuwa utumishi wa umma unaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
Pia alieleza kuhusu majukumu ya tume kuwa ni pamoja na Kumshauri Rais kuhusu masuala ya utumishi wa umma kadri atakavyohitaji, Kutoa miongozo na kufuatilia uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika Utumishi wa Umma, Kupokea na kushughulikia rufaa za mashauri yaliyotolewa maamuzi na Mamlaka za Nidhamu, Kuwezesha, kufuatilia na kutathmini utendaji kazi wa watumishi wa umma wa ngazi mbalimbali ili uwe wa ufanisi na wenye kuzingatia matokeo.
Vilevile kuwaita Watendaji Wakuu kutoa maelezo kuhusu utendaji kazi usioridhisha pale Tume inapokuwa na ushahidi au malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu, Kuhakikisha kuwa Taratibu za Uendeshaji za Utumishi wa Umma wa makundi mbalimbali zinatayarishwa na kutumika ipasavyo na Kutekeleza majukumu mengineyo kwa mujibu wa Sheria mbalimbali zilizopo.
Bi. Mollel alielezea kuhusu muundo wa tume, majukumu ya waajiri, mamlaka za ajira na nidhamu katika utumishi wa umma na kwamba tume inasimamia masuala ya rasilimali watu katika utumishi wa umma.
Aidha, alieleza matarajio ya tume kuwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu wanatekeleza maagizo ya Tume kwa wakati na kutoa taarifa ya utekelezaji wa maagizo hayo, Mamlaka za Ajira kuhakikisha kuwa ajira, upandishwaji vyeo na uthibitishwaji kazini unafanyika kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma, Mamlaka za Nidhamu zinazingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo katika kushughulikia Mashauri ya Nidhamu ili haki iweze kutendeka.
“Wakuu wa Taasisi za Umma mnao wajibu wa kuhakikisha mnawasimamia kwa karibu watumishi walio chini yenu ili waweze kutimiza majukumu yao”, alisema Bi. Mollel. Huku akiwataka wakuu hao kuhakikisha wanafanyakazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, miongozo na kuhakikisha wanafanyakazi kwa kuzingatia mipaka waliyowekewa.
Naye Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Nyakimura Muhoji aliwasihi Maafisa Utumishi kuzingatia taratibu katika upandishaji wa vyeo hasa katika kigezo cha utendaji kazi mzuri. Pia aliwasihi kuacha tabia ya kutowasikiliza watumishi walio chini yao na kuwanyanyasa kwani tabia hiyo huwa ni kero kwa watumishi.
Vilevile aliwashauri Mhe. Meya, Wenyeviti wa Halmashauri, Naibu Meya na Manaibu Wenyeviti wa Halmashauri kutenga muda pamoja na madiwani ili waweze kupata elimu juu ya Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali ambayo itakuwa ikiwasaidia kwenye usimamizi wa shughuli mbalimbali za Hamashauri.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi alipokuwa akiongea na viongozi wa Tume aliwashukuru kwa maamuzi yao ya kufanya ziara katika mkoa wa Lindi. Pia aliwasihi kuwa watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma kuwa waadilifu kwani wanafanya kazi ya kuwasimamia viongozi na watumishi wa umma.
Mhe. Zambi alieleza kuwa katika kipindi hiki kumekuwa na mabadiliko makubwa ya kiutendaji kwa watumishi wa umma kwani hata wananchi wamekuwa wakilisemea hilo. Hata hivyo bado kazi ya kuendelea kuwasimamia kuhakikisha watumishi ambao hawajabadilika wanabadilika.
Aidha, aliwaelezea fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo Mkoani Lindi zikiwemo uwekezaji mkubwa wa Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asili, Ujenzi wa Kiwanda cha Mbolea, Madini ya Graphite na Gypsum, zao la Korosho, Ufuta na Utalii (Mbuga ya Selous). Pamoja na kuwakaribisha kuja Lindi, Mhe. Zambi amewaomba viongozi wa Tume ya Utumishi wa Umma kusaidia kuutangaza Mkoa wa Lindi kwani bado watu wanamtazamo wa zamani wakati sasa kuna mabadiliko makubwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.