Wananchi watakiwa kutumia fursa ya uwepo wa madaktari bingwa kupima afya zao.
Wananchi wa Mkoa wa Lindi watakiwa kutumia vizuri fursa ya uwepo wa madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupima afya zao na kupatiwa matibabu.
Haya yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi wakati akizindua utoaji huduma za vipimo na matibabu unaofanywa na madaktari bingwa wakishirikiana na madaktari na wataalam katika hospitali ya rufaa ya sokoine, huduma ambayo inatolewa kuanzia tar. 25-30/09/2017.
Uzinduzi huu ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali ambao ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Bima ya Afya, Mhe. Anna Makinda (Spika Mstaafu), Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Ndg. Ramadhani Kaswa, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Ndg. Aifena Mramba, Wah. Wakuu wa Wilaya na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Lindi, Ndg. Mohamed Lihumbo, Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Lindi, wataalam wa NHIF, Sekretarieti ya Mkoa, hospitali ya rufaa ya sokoine na wananchi waliokuwa wamekuja kupata huduma.
Madaktari hawa bingwa wameletwa chini ya ufadhili wa Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa ambao pia wameleta vifaa tiba pamoja na madawa. Huduma zitakazotolewa ni pamoja na za magonjwa ya moyo, magonjwa ya ndani, magonjwa ya mfumo wa mkojo, magonjwa ya akina mama – kike na uzazi, magonjwa ya macho, sikio, pua na koo na magonjwa mahututi na usingizi.
Mhe. Zambi aliwaeleza wananchi waliokuwa wamefika kupata matibabu kutumia fursa hii vizuri na kuhakikisha wanawajulisha ndugu zao wenye matatizo mbalimbali ya kiafya. Ambapo pia amevisihi vyombo vya habari kuwatangazia wananchi juu ya uwepo wa madaktari hawa.
“Nimshukuru Mhe. Makinda na uongozi mzima wa NHIF kwa kufanikisha zoezi hili la upimaji afya na utoaji matibabu kunakofanywa na madaktari bingwa kwani hii inasaidia sana katika kusogeza huduma kwa wananchi wa chini ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia gharama katika kupata huduma”, alisema Mhe. Zambi.
Aidha, madaktari na watumishi wa hospitali ya rufaa ya sokoine wametakiwa kutumia fursa hii ya uwepo wa madaktari bingwa kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu utoaji huduma za afya ili wakiondoka waweze kuendelea kutoa baadhi ya huduma. Pia amemuagiza mganga mkuu wa mkoa kuvitunza vifaa vyote vitakavyoachwa na NHIF na kuhakikisha vinatoa huduma kwa wananchi.
Vilevile, Mhe. Zambi amemuagiza Katibu Tawala Mkoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, Mganga Mkuu wa Mkoa na Waganga Wakuu katika Halmashauri kuhakikisha wanatumia vizuri fursa ya mikopo inayotolewa na NHIF ya kuboresha huduma za afya ili kuimarisha utoaji huduma katika vituo.
Kabla ya uzinduzi kufanyika, Mhe. Makinda alielezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na NHIF ikiwa ni pamoja na utoaji mikopo inayosaidia katika kuboresha huduma za afya. Pia aliwasihi wananchi kujiunga na bima ya afya kwani ugonjwa hutokea muda wowote. Aidha, Mhe. Makinda aliwataka watumishi wa afya kubadilika kwani kumekuwepo na malalamiko kwa baadhi ya watumishi wa afya kutumia lugha mbaya na kutowajali wagonjwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.