Waandishi wa habari Mkoa wa Lindi wamejengewa uwezo kuhusu Mpango wa Equip – T.
Mratibu wa Mpango wa Kuboresha Elimu Tanzania (EQUIP – T) Mkoa wa Lindi, Ndg. Kasper Mmuya amewasihi waandishi wa habari kuelezea mafanikio ya mradi huo.
Waandishi wa habari walielezwa hayo katika mafunzo yaliyoandaliwa na EQUIP - T ya kuwajengea uwezo na uelewa kuhusu mradi ambayo yalifanyika wilayani Ruangwa. Katika mafunzo haya walishiriki baadhi ya waandishi wa habari wakiwemo wa ITV, Channel Ten, Mashujaa Radio, Lindi FM, Ruangwa FM, Radio One na waratibu wa mradi toka Halmashauri zote za Mkoa wa Lindi.
Ndg. Mmuya alieleza kuwa mpango huu unalenga kuongeza ubora wa elimu kwa shule za msingi na unazingatia jinsia. Katika ngazi ya mkoa mpango huu unasimamiwa na Katibu Tawala wa Mkoa akisaidiwa na watendaji wa sekretarieti ya mkoa. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ndiye msimamizi mkuu wa utekelezaji wa mpango katika ngazi ya halmashauri.
Hivyo watendaji wa halmashauri, waratibu elimu kata na walimu wakuu ndiyo watekelezaji wa shughuli zilizopangwa katika program hii kwa kushirikiana na wazazi na asasi za kiraia.
Vilevile Ndg. Mmuya alielezea malengo makuu matano ambayo mpango umejikita zaidi ambayo ni Kuongeza umahiri wa ufundishaji wa walimu kwa kuongezeka maarifa, ujuzi na ari katika utendaji kazi, Kuongeza umahiri katika usimamizi wa shule, Kuongeza umahiri katika usimamizi wa elimu katika Wilaya na mkoa, Kuongeza ushirikishwaji wa jamii katika elimu na Kuimarisha mfumo wa ukusanyaji taarifa, utunzaji na uwajibikaji.
Maeneo yote haya matano tayari yanaendelea kuwafanyiwa kazi ambapo mafunzo mbalimbali yamekuwa yakitolewa kwa makundi tofauti lengo likiwa ni kuboresha elimu ya msingi hasa kuanzia elimu ya awali, darasa la kwanza, la pili na la tatu. Vilevile Equip -T wameshatoa vifaa mbalimbali vya kufungishia ikiwa ni pamoja na kuwapatia pikipiki walimu wakuu na waratibu elimu kata.
Katika mafunzo hayo ambayo yamesaidia sana kutoa uelewa wa kutosha wa mradi wa waandishi wa habari, Ndg. Mmuya aliwaomba waandishi pale wanapokuwa wanapita kikazi katika maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa wa Lindi, kuandika habari zinazohusu matokeo ya utekelezaji wa mradi huu.
“Ni matumaini yangu kuwa, kwa kuwa mmeshapata uelewa wa kutosha kuhusu namna EQIP – T inavyotekelezwa na hatua tuliyofikia mpaka sasa, mtakuwa mstari wa mbele katika kuuelezea mradi sambamba na kuielimisha na kuihamasisha jamii ili ishiriki katika kuboresha na kusimamia maendeleo ya elimu”, alisema Mmuya.
Aidha, Ndg. Mmuya amezishauri halmashauri kuwashirikisha waandishi wa habari katika kaguzi zao mbalimbali wanazokuwa wakizifanya kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia sana katika kuweka wazi kwa umma nini kinachofanyika katika maeneo yao.kuhusu utekelezaji wa mradi.
Waandishi wa habari walipata fursa ya kutembelea kituo cha utayari cha Nachiulaga kilichopo katika Kata ya Mbekenyera Wilayani Ruangwa ambapo Ndg. Mmuya alianzisha harambee ambayo washiriki wote wa mafunzo walichangi pamoja na wanajamii waliokuwepo ikiwa na lengo la kuihamsha jamii kuona umuhimu wa kuchangia elimu.
Bi. Fatuma Maumba kutoka ITV alisema mafunzo haya yamesaidia sana kutoa uelewa wa namna mradi wa EQIP – T unavyotekelezwa. “Kutokana na maelezo yaliyotolewa sasa waandishi wa habari tumepata uelewa wa ushiriki wa kila mdau katika koboresha na kusimamia maendeleo ya elimu katika mkoa”, alisema Bi. Maumba. Pia waandishi waliomba kuwa wanashirikishwa katika vikao mbalimbali vya kujadili maendeleo ya mradi kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kuwa na uelewa wa pamoja.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.