Wadau watakiwa kuusimami Mpango Mkakati wa Elimu 2020
Wadau wa elimu mkoa wa Lindi watakiwa kukuusimamia mpango mkakati wa elimu 2020 ili kuondokana na ufaulu usioridhisha.
Wadau hao wakiwemo Viongozi mbalimbali wa serikali na taasisi zisizo za kiserikali, walimu, wazazi na wanafunzi walikutana katika Uwanja wa Ilulu wakati wa sherehe fupi za uzinduzi wa mpango mkakati wa elimu mkoa wa Lindi mwaka 2020 pamoja na utoaji tuzo kwa waliofanya vizuri katika mitihani mbalimbali ya taifa kwa mwaka 2019.
Akizungumza kabla ya kuuzindua mpango mkakati huo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi alisema kwamba mkoa umekuwa ukiweka mikakati mbalimbali ambayo pia ilishirikishwa kwa viongozi na jamii katika ngazi zote kitu ambacho kimesaidia mkoa kuongeza ufaulu katika mitihani mbalimbali ya kitaifa ya mwaka 2020.
“Mpango Mkakati huu ninaouzindua leo ndiyo dira yetu katika kuondokana na ufaulu usioridhisha kwa watoto wetu kwani mambo ya msingi ambayo yamekuwa ni changamoto katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 yamebainishwa”, alisema Mhe. Zambi.
Mkuu wa Mkoa Zambi alisema kuwa Mpango Mkakati huo umegusa mambo yafuatayo ambayo yatahitaji usimamizi na ufuatiliaji:-
Hivyo amewataka wadau wote kushirikiana katika kuhakikisha mpango mkakati huo unatekelezwa kikamilifu kwa kila mmoja kufanya ufuatiliaji katika eneo lake.
Mkuu wa mkoa Zambi pia amewapongeza wote waliopata tuzo mbalimbali kama motisha kwa kufanya kazi nzuri na kuwataka kuendeleza bidii hiyo ili mkoa uweze kufanya vizuri zaidi. Aidha, amewasihi wale ambao hawakufanya vizuri kuhakikisha wanabadilika ili kuweze kufikia malengo ambayo yamewekwa na mkoa.
Naye Afisa Elimu Mkoa wa Lindi, Vicent Kayombo alisema katika mtihani wa taifa wa kidato cha sita mkoa umekuwa wa kwanza kati ya mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani, tena kwa kutokuwa na daraja sifuri. Kwa kidato cha nne mkoa umeshika nafasi ya 23 kati ya mikoa 31 Tanzania Bara na Visiwani ambapo asilimia ya ufaulu imepanda kutoka 69.3 ya mwaka 2018 mpaka asilimia 83.2. Kwa upande wa kidato cha pili mkoa haukufanya vizuri kwani umeshika nafasi ya 26 kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Katika mtihani wa kitaifa wa darasa la saba mwaka 2019 mkoa umeshika nafasi ya 18 kutoka nafasi ya 24 mwaka 2018, ambapo ufaulu umepanda kutoka asilimia 68.71 mwaka 2018 hadi asilimia 76.48 mwaka 2019. Kwa darasa la nne mkoa umeshika nafasi ya 10 kitaifa kutoka nafasi ya 20 mwaka 2018, ambapo ufaulu umefikia asilimia 94.7 kutoka 91.96 mwaka 2018.
Kwa upande wa walimu ambao shule zao au walimu wao wamepata tuzo, wameupongeza uongozi wa mkoa kwa kuamua kuandaa sherehe hizo ambazo zimewafanya walimu kutoka maeneo mbalimbali ndani ya mkoa kuweza kukutana na kupongezana kwa pamoja. Aidha, wameahidi kurudi kuendelea na kazi wakiwa na nguvu mpya na kwamba wapo tayari kupambana kuhakikisha mkoa unaendelea kunyanyuka kiufaulu.
Sherehe hizi za utoaji tuzo zitakuwa zikifanyika kila mwaka ambapo wale waliofanya vizuri watapewa tuzo na fedha kama motisha na kwa wale watakao kuwa wamefanya vibaya kupatiwa bendera nyeuzi ambazo zitatakiwa kusimamishwa ndani ya ofisi zao lengo likiwa ni kuwakumbusha juu ya matokeo mabovu waliyoyapata na kwamba wanahitaji kuongeza jitihada.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.