Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Bw. Majid Myao akiwa mgeni rasmi kwenye warsha ya uhamasishaji wa falsafa ya KAIZEN kwa wazalishaji na watoa huduma wa Lindi, amewataka wamiliki wa Viwanda na Wajasiriamali kuifanya Kwa vitendo Falsafa ya KAIZEN.
Akiwahutubia wadau waliojitokeza kwenye warsha hiyo iliyofanyika tarehe 24 Mei, 2023 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bw. Myao amesema kuwa falsafa ya KAIZEN inaimarisha mfumo wa uzalishaji na utoaji wa huduma bora.
Bw. Myao ameongeza kuwa kupitia falsafa hii uzalishaji na utoaji wa huduma utakuwa na tija na utachochea maendeleo ya mmoja mmoja, taasisi pamoja na Mkoa kwa ujumla.
Nae Mkuu wa Kitengo cha KAIZEN kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Bw. Richard Pweleza amesema kuwa lengo la warsha hii ni kuwahamasisha wadau ili waweze kujisajiri na kupatiwa rasmi mafunzo ya falsafa ya KAIZEN.
Bw. Pweleza ameongeza kuwa lengo kuu la kuanzisha Falsafa ya KAIZEN nchini Tanzania mwaka 2013 lilikuwa ni kuboresha uzalishaji wa bidhaa na huduma katika viwanda.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dkt. Bora Haule amesema kuwa falsafa ya KAIZEN imekuja kwa muda muafaka katika mkoa wa Lindi ambao umezungukwa na fursa mbalimbali.
Dkt. Bora ameendelea kwa kuwataka wajasiliamali, wazalishaji wadogo, wakubwa na wafanyabiashara wote kuipokea falsafa ya KAIZEN ili iwaandae kuzipokea fursa za miradi mikubwa ya uchakataji wa gesi asilia, LNG, Kampuni za madini pamoja na ujenzi wa bandari kubwa ya uvuvi ambazo zinaanza muda mfupi ujao katika Mkoa wa Lindi.
Warsha ya uhamasishaji wa falsafa ya KAIZEN imefanyika mkoani Lindi ikiendeshwa na wataalam kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na biashara ikiwahusisha wadau mbalimbali ikiwemo watoa huduma za Benki, SIDO, wajasiliamali, wazalishaji wa chumvi na wengine.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.