Wafanyakazi timizeni wajibu ndipo mdai haki
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi amewataka watumishi kutimiza wajibu wao katika kutoa huduma kwa wananchi na katika kutekeleza majukumu mengine ya taasisi zao.
Agizo hili amelitoa wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Meimosi) ambapo kimkoa zilifanyika katika Viwanja vya Mkapa Garden Wilayani Kilwa.
“Wafanyakazi mnao wajibu mkubwa wa kusimamia na kutekeleza shughuli mbalimbali zinazoratibiwa na taasisi zenu, ili wananchi wa Lindi na taifa kwa ujumla wasonge mbele kimaendeleo”, alisema Mhe. Zambi. Aliendelea kwa kusisitiza kuwa haki na wajibu ni vitu ambavyo vinakwenda pamoja.
Mhe. Zambi alisema kuwa serikali inazitambua changamoto mbalimbali walizonazo watumishi na inaendelea kuzifanyia kazi. Pia aliwaagiza waajiri kuhakikisha wanaimarisha mahusiano mahala pa kazi na kuhakikisha wananunua vitendea kazi kwa watumishi ili waweze kutimiza majukumu yao.
Kutokana na tatizo la mikataba kwa watumishi wa sekta binafsi, Mhe. Zambi aliwaagiza waajiri wote wa sekta binafsi kuhakikisha wanawapatia mikataba ya kazi watumishi wao pamoja na kupeleka fedha za michango yao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Pia aliwaagiza waajiri wote kuhakikisha wanaandaa taarifa za wastaafu na kuziwasilisha kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa wakati ili maadalizi ya malipo ya mafao yaweze kufanyika kwa wakati. Katika hili pia aliwashauri wale wote ambao wanaelekea kustaafu kuanza kuzihakiki taarifa zao mapema kukwepa usumbufu.
Aidha, Mhe. Zambi aliwaeleza watumishi kuwa maandalizi ya maisha ya kustaafu huwa yanaanza mara tu mtumishi anapopata ajira hivyo ni vema wale ambao muda wao wa kustaafu haujafika wakajiandaa badala ya kusubiria fedha za mafao.
Vilevile watumishi na jamii walishauriwa kujenga mahusiano mazuri kwani kwa kufanya hivyo wataweza kushirikiana vizuri katika shughuli za maendeleo. Pia amewashauri watumishi na jamii kwa ujumla kuwa na tabia za kupima afya zao ikiwa ni pamoja na kushiriki mazoezi kwani yanasaidia kiafya.
Watumishi pia wameshauriwa kutosubiri Meimosi ili kuwasilisha matatizo waliyonayo badala yake wayafikishe kwa viongozi pindi matatizo au changamoto zinapojitokeza. Mhe. Zambi amevipongeza vyama vya wafanyakazi kwa kufanikisha kufanyika kwa maadhimisho haya na kuwaahidi kuwa serikali itaendelea kuwapa ushirikiano na itaendelea kutatua changamoto za watumishi.
Naye Katibu wa TUCTA Mkoa wa Lindi, Fatuma Chionga aliposoma taarifa ya kwa niaba ya wafanyakazi alisema kuwa wafanyakazi licha ya kutimiza majukumu waliyonayo, wanaza changamoto zinazowakabili zikiwemo kupandishwa mishahara, vyeo, na uchache wa vitendea kazi.
Katika sherehe hizi watumishi hodari kutoka katika taasisi mbalimbali ndani ya Mkoa walikabidhiwa zawadi zao na Mkuu wa Mkoa huku wakisisitizwa kwenda kuongeza bidii zaidi ili ikiwezekana mwakani wapate tena.
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani kwa Mkoa wa Lindi yalihudhuriwa na Katibu Tawala Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Meya na Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi, Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi, Watumishi kutoka taasisi mbalimbali na wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.