Wafanyakazi watakiwa kujitathmini
Wafanyakazi mkoani Lindi wametakiwa kutumia siku ya MEIMOSI kutathmini utendaji wao wa kazi ili kuona kama wanatimiza wajibu wao ipasavyo.
Wafanyakazi walielezwa hayo na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani 1 Mei, 2019 ambayo kimkoa yalifanyika katika viwanja vya shule ya msingi mpilipili – manispaa ya Lindi.
Zambi aliwaeleza wafanyakazi kuwa siku ya meimosi inatoa fursa kwao kujitathmini kiutendaji, na kubaini vitu ambavyo vinaweza kuwa ni chanzo cha kuwakwamisha katika utendaji wao.
“Ni vema sote kwa pamoja tukajitafakari kama ni kweli tunatimiza wajibu wetu katika pande zote kwa maana ya waajiri na wafanyakazi kwani kila upande ukitimiza wajibu wake hakuna kitakachoshindikana”, alisema Zambi.
Wafanyakazi walielezwa kuwa serikali kwa upande wake inatambua changamoto walizonazo na tayari imeshaanza kuzifanyia kazi ikiwemo ya upandishaji madaraja na ulipaji wa madeni ya watumishi.
Pia aliwataka viongozi kuhakikisha wanaboresha ushirikiano na mshikamano baina yao na watumishi walio chini yao kwani kwa kufanya hivyo ndio kutasaidia kuondoa malalamikoa na manung’uniko kati yao wenyewe pamoja na watumishi wao.
Vilevile ametaka waajiri binafsi na wa taasisi zisizo za kiserikali kuzingatia haki na stahiki za wafanyakazi wao kwa kulipa maslai ya wafanyakazi wao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, kwani kumekuwepo na malalamiko ya kutozingatia hilo.
Aidha, waajiri wote wametakiwa kuhakikisha michango ya watumishi inayokwenda kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii inapelekwa kwa wakati. Hili ni sambamba na kuhakikisha nyaraka zote muhimu za wastaafu zinakamilishwa kwa wakati ili mtumishi anapofikia ukomo mafao yake yapatikane kwa wakati.
Pia waajiri wote wametakiwa kusimamia vigezo vinavyotumika katika kumpata mfanyakazi hodari ili watu waache kupeana kwa kufuata nani mwaka jana kapata mwaka mwingine apate mwingine. Lengo hapa libaki ni kumpata mfanyakazi hodari, hivyo hata kama mtu amepata mara tatu na anasifa basi apate huyo huyo na si kupeana bila kuangalia vigezo.
Zambi amewataka watumishi kuwa na imani na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwani inashughulikia na inaendelea kusimamia haki na stahiki za watumishi. Hivyo amewasihi watumishi kuendelea kuchapa kazi kwa kila mmoja kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na maadili ya kazi yake.
Naye mratibu wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi (TUCTA) Bi. Fatma Chiwonga amewaomba waajiri kuwasaidia wastaafu kupata mafao yao kwa wakati kwani kumekuwepo na tatizo la kutokamilika kwa nyaraka zinazotakiwa kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kuyafuatilia katika mifuko husika.
Vilevile aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza makato ya kodi kwa watumishi kupitia mishahara ambayo kwa sasa wanakatwa asilimia 9 na kuomba ishuke mpaka asilimia 6 kwani wafanyakazi wengi wanaishi katika mazingira magumu.
Maadhimisho hayo yamebeba ujumbe wa "Tanzania ya uchumi wa kati inawezekana wakati wa mishahara na maslahi bora kwa wafanyakazi ni sasa".
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.