Akizungumza kwenye mkutano uliojumuisha wakulima na wafugaji uliofanyika jana tarehe 18 Juni 2021 eneo la shule ya msingi Nangurukuru iliyopo wilayani Kilwa, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab R. Terack ameyataka makundi hayo mawili kudumisha amani katika shughuli zao za maerndeleo. Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wataalam mbalimbali wa serikali ziliibuliwa hoja nyingi za migogoro zikielekezwa pande zote mbili ikiwemo kuuawa kwa mfugaji kijiji cha Njinjo, Kilwa na kuuawa mifugo.
Mgogoro mkubwa ulielekezwa kwa wafugaji wakituhumiwa kulisha mazao ya wakulima na kusababisha hasara kubwa ambayo hata hivyo malipo yake huwa hayaendani na dhamani ya mazao husika. Kundi la wakulima limeonekana kuchoshwa na vitendo vya wafugaji hao kuwasababishia hasara lakini wanapohoji huambulia kipigo kutoka kwa wafugaji. "Ki ukweli sie hatuwawezi kwa sababu wao wanatumia fimbo na sime." mmoja wa wakulima alieleza.
Mfugaji Donald Robert alieleza mbele ya mkutano kuwa chanzo kikubwa cha migogoro ya wafugaji na wakulima ni uhaba wa maji hasa kipindi cha kiangazi. Aliendelea kueleza kuwa, kipindi cha kiangazi wafugaji wengi huelekea mto mbwemkulu ambako hukutana na shughuli za kilimo cha umwagiliaji jambo ambalo huibuia migogoro. Pamoja na ukame bwana Donald aliongezea kuwa sababu nyingine ya wafugaji kuhama hama ni vitendo vya uchomaji moto kiholela kitendo ambacho huharibu malisho. Mfugaji huyo alienda mbali kwa kuiomba Serikali kutengeneza miundombinu ya maji kwa ajili ya mifugo na kuondoa changamoto zinazojitokeza.
Mhe. Zainab R. Telack amewataka wafugaji na wakulima kufanya shughuli zao kwa maslahi ya uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla huku wakizingatia taratibu zilizowekwa na serikali. Mhe. Mkuu wa Mkoa alionesha masikitiko yake kuhusiana na vyanzo vya migogoro inayojitokeza hasa vitendo vya rushwa kwa viongozi wa vijiji, uchomaji moto wa misitu na pembezoni mwa barabara. Katika kuhakikisha migogoro inakoma, Mkuu wa Mkoa amewataka wafugaji kuchimba malambo ya kunyweshea mifugo yao na kuacha vitendo vya kuhama hama huku akipiga marufuku uingizaji wa mifugo mipya ndani ya mkoa. "Sitaki mifugo mipya, sitaki wafugaji wapya na wafugaji waliohamia mkoa wa pwani wasirudi tena." alisema akimuelekeza Kamanda wa Polisi Wilaya na Afisa Usalama Wilaya kusimamia hilo.
Mkuu wa Mkoa amewataka watendaji wote kuwajibika kwa kuchukua hatua kwa vitendo vinavyochochea migogoro kwenye jamii. Aliwataka viongozi wa vijiji kukomesha uchomaji moto kiholela kwa kuwachukulia hatua wahusika na kiongozi atakaeshindwa kudhibiti suala la moto Kamanda wa Polisi Wilaya ashughulike nae.
Makundi ya wafugaji na wakulima ni makundi muhimu sana kwenye uchumi na maendeleo ya mkoa, hivyo ni lazima kwa serikali kuchukua hatua pale ambapo kunahitaji nguvu eidha ya kimaendeleo au kuweka mambo sawa. Mkuu wa Mkoa wa Lindi ameendelea na ratiba yake ya kukutana na kuzungumza na makundi mbalimbali ndani ya mkoa wake.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.