Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Ndg. Ngusa Samike amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya barabara katika wilaya ya Kilwa kuhakikisha wanatumia ipasavyo fedha za serikali zinazotolewa kwa ajiri ya utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na kuhakikisha wanatekeleza miradi hiyo kwa wakati kama ilivyoelekezwa katika mikataba yao ili kutimiza adhima ya serikali ya kuweka miundombinu rafiki ya usafirishaji wa watu na bidhaa.
Katibu Tawala ametoa rai hiyo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya barabara inayotekelezwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini {TARURA} kwa mwaka wa fedha 2022/2023, ambapo amewataka wakandarasi kuacha kutoa visingizio wanaposhindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati kulingana na mikataba yao ya kazi.
“Na hawa wakandarasi tunataka tu tuwape onyo, na sasa hivi tutakua na utaratibu kama mkandarasi anashindwa kazi hatutataka kumuona akipewa kazi tena katika mkoa wetu, na sio tu kama tutachukua jina,tutachukua hadi na namba ya vifaa anavyotumia ili ikitokea anakuja kuomba tena kazi kwa kutumia jina lingine la kampuni aliloisajiri upya tuweze kumfahamu’’amesema Katibu Tawala.
Aidha, Katibu Tawala Mkoa alipotembea barabara ya Mingumbi- Chapita yenye urefu wa KM 12 inayofanyiwa matengenezo na Mkandarasi M/S MALCOM INVESTMENT CO.LTD na kugharimu kiasi cha Tsh. Milioni 390, amewataka TARURA wilaya ya Kilwa kumsimamia kwa karibu mkandarasi huyo aweze kukamilisha kazi yake kwa wakati kabla ya msimu wa mvua kuanza.
“Sijaridhishwa kwa ujumla na kasi ya ujenzi, hii barabara ina umuhimu wake mkubwa kutokana na uzalishaji mkubwa unaofanyika katika maeneo haya na barabara hii ndio inategemewa kwa usafirishaji wa idadi kubwa ya watu wanaoishi katika vijiji hivi pamoja na mazao yao wanayoyazalisha, sasa nawasisitiza mumsimamie kwa karibu mkandarasi ili akamilishe hii barabara kabla ya mvua zinazoanza mwezi wa nne maana hii barabara haitopitika”
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi ya barabara, Meneja wa TARURA wilaya ya Kilwa Mhandisi Agatha Mtwangambate ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 wilaya ilitengewa kiasi cha Tsh Milioni 918 kutoka katika fedha za mfuko wa barabara {Road Fund} kwa ajiri ya matengenezo ya barabara na Makalvati.
“kwa mwaka wa fedha 2022/2023 TARURA tumeweza kuingia mikataba 12 na wakandarasi mbalimbali kwa kazi za ujenzi wa madaraja, makalvati na matengenezo ya barabara kupitia fedha za mfuko wa barabara na za maendeleo, aidha hadi kufikia februari 2023 mikataba 11 imesainiwa na wakandarasi wote wameanza kazi ambapo wakandarasi watatu wamekamilisha kazi kwa asilimia 100, na mkataba mmoja upo katika hatua ya manunuzi” Mhandisi Agatha.
Wilaya ya Kilwa ina Mtandao wa Barabara zenye urefu wa Kilomita 1,079.10 ambazo zinahudumiwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini {TARURA}, Mtandao huu umegawanyika katika sehemu tatu ambazo ni Barabara Wilaya zenye jumla ya urefu wa km 559.66, Barabara za vijiji zenye urefu wa km 353.08 na Barabara za jamii zenye jumla ya km 166.3
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.