Wakazi wa Lindi wanavyoboreshewa huduma za jamii
MKOA wa Lindi ulianzishwa rasmi Julai mosi, 1971, baada ya Mkoa wa Mtwara kugawanywa, mkao makuu yake yapo Mji wa Lindi. Mkoa huu una eneo la kilomita za mraba 67,000. Hata hivyo, asilimia 27 ya eneo la mkoa huu lipo chini ya Mbuga ya Selous “Selous Game Reserve” ambayo ipo Magharibi mwa Wilaya ya Liwale.
Mkoa wa Lindi unapakana na Bahari ya Hindi kwa upande wa Mashariki, upande wa Kaskazini, umepakana na Mkoa wa Pwani, Magharibi umepakana na mikoa ya Morogoro na Ruvuma na Kusini unapaka na Mkoa wa Mtwara.
Kiutawala Mkoa wa Lindi una wilaya 5 ambazo ni; Lindi, Ruangwa, Nachingwea, Liwale na Kilwa. Pia una halmashauri 6 ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Halmashauri za Wilaya za Lindi, Kilwa, Nachingwea, Liwale na Ruangwa.
Pia mkoa huu una tarafa 28, kata 150, mitaa 117 na vijiji 536 vilivyoandikishwa, miji midogo 3 ambayo ni Kilwa Masoko, Kilwa Kivinje na Nachingwea. Mkoa huu una majimbo 8 ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, Lindi ina wakazi 864,652, wanaume 414,507 na wanawake 450,145. Makabila ya asili ya mkoa huu ni Mwera, Makonde, Ngindo, Matumbi na Machinga.
Kwa upande wa afya mkoa una jumla ya hospitali 9, vituo vya afya 19 na zahanati 205.
Mkoa umeendelea kuimarisha huduma za afya, ambapo miundombinu ya Hospitali ya Rufaa ya mkoa imeendelea kuimarishwa pamoja na hospitali za wilaya. Vituo vya afya na zahanati vimeendelea kujengwa na kuboreshwa lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Akizungumzia kuhusu ukarabati uliofanywa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (Sokoine), ambayo ilijengwa mwaka 1954, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi anasema kuwa ukarabati umefanyika katika wodi namba 5 na 6 na wodi maalumu (executive ward) na ujenzi wa kichomea taka cha kisasa.
“Mkoa umepanga kufanya ukarabati wa vyoo 9 vya wagonjwa na watumishi kati ya Aprili na Juni, 2018. Pia, miundombinu ya maji inaboreshwa katika wodi na vyoo, ujenzi wa kisima cha chini cha lita 150,000 na tenki la juu la lita 50,000 ambapo utekelezaji wake ni kati ya Aprili na Juni, mwaka huu,” anasema Zambi.
Pia, anaeleza kuwa hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa sasa ni nzuri hadi kwenye ngazi ya zahanati, wananchi vijijini wanapata huduma ya afya licha ya changamoto ya upungufu wa watumishi.
Mkuu huyo wa mkoa, anasema kuwa katika kuhakikisha huduma za afya zinaimarishwa na kusogezwa jirani na wananchi, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wametoa Sh. Bilioni 6.2 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu kwenye vituo vya afya 12. Kazi zilizotakiwa kufanyika ni pamoja na ujenzi wa majengo ya maabara, jengo la mama na mtoto, jengo la upasuaji, jengo la kuhifadhia maiti na nyumba ya daktari.
Anasema kuwa katika kutekeleza ukarabati na ujenzi huo, fedha zilitolewa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza zilitoka shilingi bilioni 1.5, kwa vituo vya Nyangamara, Kilwa Masoko na Nkowe. Ambapo kila kituo kilipata Sh. milioni 500, kazi ya ukarabati na ujenzi katika vituo hivyo umeshakamilika, kinachoendeleani ufungajiwa vifaa.
Aidha, katika awamu ya pili zilizotolewa Sh. bilioni 4.7 ambapo Kituo cha Afya Pande kimepewa Sh. milioni 400, Tingi Sh. milioni 400, Kibutuka Sh. milioni 400, Mpengere Sh. milioni 600, Kilimarondo Sh. milioni 400, Mbekenyera Sh. milioni 500 na Mandawa Sh. milioni 400.
Pia, Kituo cha Afya Mnazi Mmoja kilipatiwa Sh. Bilioni 1.1 na Kitomanga Sh. milioni 400. Kazi za ujenzi katika vituo vyote hivi inaendelea kwa kutumia mafundi wadogo wa ndani wakishirikiana na wananchi wa maeneo husika.
Naye, Katibu Tawala Msaidizi - Afya, Dk. Genchwele Makenge anaeleza kuwa sekta ya afya katika mkoa inashirikiana na wadau mbalimbali wa afya ambao ni Usaid Boresha Afya, GIZ, Chai. Ima World Health, SIGTH Savers, Marie Stops, VSO na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef).
“Wadau hawa wanashiriki kutoa huduma mbalimbali zikiwemo za afya ya mama na mtoto, chanjo, ugawaji dawa za kujikinga na matende, minyoo na ngiri maji, uzazi wa mpango, lishe, kudhibiti ugonjwa wa kifua kikuu, huduma ya madini joto, malaria na udhibiti wa Maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi,” anasema Dk. Makenge.
Katika utoaji huduma ya elimu, mkoa una jumla ya shule za msingi 503, shule za sekondari 123 na shule 8 za kidato cha tano na sita. Pia, vipo vituo vya Memkwa 50 na vituo vya ufundi stadi 13.
Akizungumzia kuhusu hali ya ufaulu Katibu Tawala Msaidizi – Elimu, Wengi Mchuchuri anasema katika matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la saba mwaka 2017, mkoa ulishika nafasi ya 14 na kwa upande wa kidato cha nne mkoa ulishika nafasi ya 27.
“Kwa ujumla matokeo kwa upande wa sekondari hayakuwa mazuri jambo ambalo lilimfanya mkuu wa mkoa kufanya vikao vya wadau wa elimu katika kila halmashauri ili kupata ufumbuzi wa namna ya kuongeza ufaulu,” anasema Mchuchuri.
Mchuchuri anasema kuwa katika vikao vilivyofanyika yalitolewa maelekezo ambayo viongozi katika wilaya na halmashauri walielekezwa kuyasimamia. Maelekezo haya yanagusa majukumu ya wazazi/walezi, wanafunzi, walimu, kamati/bodi za shule na viongozi kuanzia ngazi ya mkoa hadi kijiji.
Aidha, sekta ya elimu inasimamia na kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu chini ya mpango wa EQUIP – T. Kwa mwaka 2018 mkoa umepokea fedha kiasi cha Sh. 1,075,887,910 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za mafunzo kwa walimu na ujenzi wa shule shikizi na umaliziaji wa maboma katika shule za msingi.
Maji
Kuhusu sekta ya maji uongozi wa mkoa wa Lindi umebainisha kuwa unatekeleza miradi ya maji katika vijiji 10 kwa kila halmashauri, ambapo mpaka sasa jumla ya miradi 37 ujenzi wake umekamilika na kutumika, miradi miwili ujenzi upo katika hatua za mwisho kukamilishwa na miradi yote itakapokamilika jumla ya vijiji 71 vitanufaika na huduma ya maji.
Pia mkoa unatekeleza Mpango wa maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya II (WSDP II) chini ya programu ya maji na usafi wa mazingira vijijini (RWSSP) katika vijiji 76. Hadi kufikia Machi, 2018, Miradi katika vijiji 28 Usanifu umekamilika na utekelezaji wake utaanza hivi kiribuni, Hivyo vijiji 369 kati ya vijiji 540 vinapata maji safi na salama. Katika baadhi ya vijiji huduma inayopatikana bado haitoshelezi mahitaji halisi kulingana na idadi ya watu. Huduma ya maji inayopatikana kwa sasa ni asilimia 54.5.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Maji, Mhandisi Valentine Ndyano anasema kuwa kwa upande wa maji safi na salama katika mji wa Lindi na miji mikuu ya wilaya imefikia asilimia 65.2
Vilevile katika kuhakikisha miradi ya maji inakuwa endelevu, miradi yote inaendeshwa na wananchi wenyewe kupitia vyombo/vikundi huru vya watumiaji maji vinavyoundwa kisheria (COWSOs). Ambapo mkoa una jumla ya vyombo vya watumiaji maji 145 vilivyoanzishwa na kusajiliwa.
Anabainisha kuwa katika Manispaa ya Lindi, mradi wa maji wa Ng’apa upo hatua za mwisho za kukamilishwa na baadhi ya mitaa imeanza kupata huduma ya maji. Mradi huo ambao umegharimu zaidi ya Sh. Bilioni 29 utazalisha maji lita milioni 7.5 kwa siku wakati mahitaji ya maji kwa siku ni lita milioni 5. Mamlaka ya Maji Lindi (Luwasa) kwa sasa inaendelea kuimarisha miundombinu ya usambazaji maji mjini ili wananchi wengi waweze kupata huduma hiyo muhimu.
Aidha, mkoa unaendelea kupanda katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, ambapo kwa upande wa mazao ya chakula yanayolimwa ni mahindi, mtama, mazao jamii ya mikunde, muhogo, mpunga na viazi vitamu. Mazao ya biashara ni korosho, ufuta, nazi, karanga, vitunguu na nyanya.
Kimsingi katika mkoa wa Lindi, zao kuu la biashara ni korosho likifuatiwa na ufuta. Kwa upande wa zao la korosho msimu wa 2017/2018, zilikusanywa na kuuzwa kilo 75,730,071 zenye thamani ya shilingi 295,612,487,333. Kupanda huko kwa mauzo ya korosho kumesaidia kuboresha maisha ya wananchi hususan waishio vijijini.
Ili kuongeza uzalishaji wa zao la korosho, mkoa umezalisha zaidi miche milioni 4, na tayari zaidi ya miche milioni tatu zimeshapandwa. Kwa kuwa eneo la kilimo bado lipo kubwa, mkoa utaendelea kuzalisha na miche mipya ya mikorosho lengo likiwa ni kuufanya mkoa kuwa mkoa wa korosho.
Kwa upande wa sekta ya ardhi mkoa wa Lindi umeendelea na upimaji wa viwanja katika miji ya halmashauri kwa lengo la kukabiliana na tatizo la ujenzi holela, ambapo kwa mwaka 2017/2018, tayari zaidi ya viwanja 15,000 vimeshapimwa na huku vingine vikiwa vimejengwa tayari. Pia hati miliki za viwanja zinaendele kutolewa ambapo mpaka sasa jumla ya hati miliki zaidi ya 7,000 za viwanja na hatimiliki zaidi ya 1,000 za kimila zimeshatolewa.
Katika kukabiliana na migogoro ya ardhi, Katibu Tawala Msaidizi – Ardhi, Jerome Kiwia anasema kuwa mkoa umeanzisha madawati ya kushughulikia kero, malalamiko, madai na fidia ya ardhi katika halmashauri zote za mkoa wa Lindi. Aidha, hadi kufikia nusu ya mwaka 2017/2018, halmashauri zilishughulikia aina mbalimbali za migogoro ya ardhi 168.
Vilevile vijiji 164 kati ya 536 tayari vina mpango wa matumizi bora ya ardhi na mkakati wa kuhakikisha vijiji vilivyobaki vinakuwa na mpango huu unaendelea.
Mkoa wa Lindi kwa upende wa barabara una mtandao wenye urefu wa Km. 5,108.87 kati ya hizo, barabara Km. 406 zimejengwa kwa kiwango cha lami (Paved) na barabara Km. 4,705.93 zimejengwa kwa kiwango cha changarawe na udongo (Unpaved).
Wakala wa barabara Mkoa (Tanroad) unahudumia mtandao wa barabara zenye urefu wa km. 1,293.34, ambapo barabara kuu ni km. 348.18 na barabara za mkoa km. 945.16. Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) unahudumia mtandao wenye urefu wa km. 3,815.53 kati ya hizo km. 18.7 ni barabara za lami na km. 3,796.83 ni za changarawe.
Katika Sekta ya Nyumba na Makazi, Meneja wa Shirika la Nyumba Mkoa wa Lindi, Gibson Mwaigomole anasema kwa mwaka 2016/2017 shirika limefanikisha na kukamilisha ujenzi wa nyumba 30 za makazi za gharama nafuu katika eneo la Mtanda ambazo nyingi zimenunuliwa na wakazi wa Mkoa wa Lindi.
Pia Shirika la Nyumba limeweza kufundisha vijana 240 katika wilaya zote za mkoa jinsi ya kutumia mashine za kutengeneza matofali yakufungamana (interlocking blocks) na jinsi ya kujenga nyumba kwa kutumia matofali hayo.
Umeme
Kwa upande wa umeme, kimejengwa kituo kikubwa cha kupoozea umeme kwenye Kijiji cha Mahumbika katika Halmashauri ya Wilaya ya Lindi. Kituo hiki ambacho kimegharimu Sh. Bilioni 16 kilianza kujengwa mwaka 2016 kimeshakamilika tangu Agosti, 2017 na kinaendelea kutumika. Hivyo, kwa sasa umeme unatoka moja kwa moja kutoka kwenye kituo cha uzalishaji kilichopo Mtwara kuja kwenye kituo cha Mahumbika tofauti na awali ambapo Mkoa wa Lindi ulikuwa unapata umeme kama sehemu ya wilaya ya Mtwara.
Kituo hiki kinapooza umeme kutoka Kilovoti 132 kwenda 33 kilovoti umeme ambapo unasambazwa katika Wilaya ya Lindi, baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Kilwa, Ruangwa, Nachingwea na Masasi. Mpango unaoendelea sasa ni kuunganisha umeme huo uweze kutumika katika Wilaya ya Liwale ambayo kwa sasa inatumia umeme wa jenereta.
Vilevile Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) Awamu ya Tatu, sehemu ya kwanza unaendelea, ambapo vijiji 144 vitapatiwa umeme na vijiji 206 vilivyobaki vitasambaziwa umeme wakati wa utekelezaji wa sehemu ya pili na awamu ya tatu itakayomalizika mwaka 2021. Hivyo awamu hii ya tatu ikikamilika vijijivyote 540 vitakuwa vimepata umeme.
Katika kutatua changamoto ya usafiri kwa wakazi wa Kitunda, ahadi ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati wa kampeni mwaka 2015 ya kujenga maegesho ya kivuko na kuleta kivuko kwa ajili ya wakazi wa eneo hilo katika Manispaa ya Lindi imeshatekelezwa. Kwa sasa wananchi wakiwa na vyombo vyao vya usafiri wanavuka salama kwa kutumia kivuko hicho kilichogharimu Sh. Bilioni 1.9.
Kabla ya kivuko hiki kuletwa wananchi walikuwa wanavuka kwa kutumia mitumbwi na wenye magari walikuwa wanalazimika kwenda kilomita 90 ili wafike Kitunda. Kivuko hiki kina uwezo wa kubeba abiria 100, magari madogo 6 na uwezo wake ni kubeba tani 50. Kwa siku kinabeba abiria 1,080.
Mkoa wa Lindi unazo fursa za kutosha kwa ajili ya kuanzisha viwanda vikubwa, vya kati na vidogo. Fursa hizo ni pamoja na kuwepo kwa uzalishaji mkubwa wa mazao ya Biashara hususani Korosho na Ufuta ambapo vitahitajika viwanda vya kubangua korosho, usindikaji mafuta ya ufuta, chakula cha mifugo na uwezekano wa kuwa na viwanda vya kutengeneza madawa ya kuua wadudu waharibifu wa mazao kwa kutumia maganda ya korosho.
Pia kutokana na uwepo wa bahari zipo fursa za uwekezaji katika uvuvi, viwanda vya kusindika samaki, kilimo cha Mwani na uvunaji wa Chumvi, viwanda vya chumvi na mazao mengine ya bahari. Aidha, uwepo wa madini mbalimbali kama vile Jasi, Risasi (Graphite) na Gesi asilia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.