Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania( TFRA) kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi imefanya uzinduzi wa Mashamba Mfano katika kijiji cha Mnolela, Halmashauri ya Mtama yatakayotumika kuhamasisha na kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea kwa kilimo chenye tija na endelevu.
Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Dkt. Stephano E. Ngailo ameeleza kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara inaongoza kwa matumizi madogo ya mbolea na utafiti umebaini kuwa sampuli za udongo zilizochukuliwa zinanyesha udongo una virutubishi pungufu vya naitrojeni, fosforasi, potasiumu na virutubishi vingine vidogovidogo (micro nutrients) kwa kiwango kikubwa.
“Upungufu huu wa virutubisho unachangia sana katika uzalishaji mdogo wa mazao ya biashara na chakula kama vile mahindi na mengineyo. Kutokana na hali hii ndio maana TFRA imeamua kutimiza jukumu lake la kushirikiana na Halmashauri za wilaya katika mikoa hii ili kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji.” alisema Dkt. Ngairo.
Mkuu wa wilaya ya Lindi Mh. Shaibu Ndemanga amewataka wananchi kuchangamkia fursa ya kwenda kupata mafunzo kwa vitendo kuhusu umuhimu na namna nzuri ya kutumia aina mbalimbali za mbolea ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao. Pia, amewataka Maafisa kilimo wa Wilaya kutoka katika Halmashauri kuendeleza mafunzo haya kwa wakulima waliopo katika halmashauri zao.
“Napenda kutumia fursa hii kuwahimiza wakurugenzi wa halmashauri zote za Lindi kutenga fedha kwenye bajeti zenu za kuanzisha, kuziendeleza na kugharamia mashamba mfano ya matumizi ya mbolea kwenye maeneo yenu” alisema Mh. Ndemanga.
Aidha, Mh. Ndemanga amehitimisha kwa kuwataka TFRA kuhakikisha kuwa maeneo yaliyotengwa yanatumika ipasavyo kwa kutoa elimu na hamasa kwa wakulima.
“TFRA isaidie upatikanaji wa mbolea kwa urahisi na kwa bei rasmi kwani yapo manung’uniko kutoka kwa wauzaji wa pembejeo kulalamika ugumu wa upatikanaji wa mbolea kwa bei elekezi ya serikali na kusababisha mbolea inayoletwa kuuzwa kwa bei kubwa, tunaomba pia TFRA kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka ya pembejeo ili kuhakikisha wakulima wanapata mbolea kwa bei halali.” Aliongeza Mh. Ndemanga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.