Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amewataka wakulima na wavuvi kuingia katika vyama mbalimbali vya ushirika kwa lengo la kujenga umoja,kuongeza vipato vyao na kupata uongozi utakaoenda kutetea haki na maslahi ya shughuli zao wanazozifanya.
Mhe. Telack ameyasema hayo wakati wa hafla ya Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika katika Mkoa wa Lindi lililofanyika siku ya Alhamis Mei 18, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Sea View Resolt.
“Lengo la kujiunga katika vyama hivi vya ushirika ni kutengeneza umoja wa kutetea maslahi yetu, tukiwa na umoja hatuwezi kuuza mazao yetu kwa bei ya hasara au ya kupangiwa na mnunuzi kama wote tutakua na kauli moja katika namna na bei ya kuuza mazao yetu, lakini kupitia vyama vya ushirika tunapata kujifunza namna mbalimbalia ya kusimamia mazao yetu ili yapate kuwa na thamani sokoni, namna nzuri ya uhifadhi na matumizi ya fedha pamoja na kuirahisishia serikali kupata takwimu sahihi za wakulima wanaohitaji kupata pembejeo za kilimo”
Aidha, Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa wanatamani sana zao la Mbaazi lingeingizwa katika mfumo wa stakabadhi ghalani ili wakulima wa mbaazi katika Mkoa wa Lindi nao waweze kunufaika kwa kupata pembejeo lakini pia kuwezesha upandaji wa bei ya zao la mbaazi sokoni ili wakulima wake waweze kunufaika kutokana na zao hilo.
Pia, Mhe. Telack ameongeza kuwa Uaminifu na Uadilifu tu ndio unaowaweka salama viongozi wa ushirika na wakulima salama hivyo amewataka kuacha vitendo viovu vinavyodhorotesha Maendeleo ya Ushirika ndani ya Mkoa wa Lindi.
“Niwatake viongozi wetu tuliowachagua katika vyama vyetu vya msingi na vyama vya ushirika muende mkatusimamie vizuri , msijihusishe na vitendo vya udanganyifu, ile tabia ya mkulima ameleta korosho au ufuta wake ghalani ukiwa safi grade one mnakuja mnachanganya na korosho chafu mnawaumiza wakulima wetu, na sisi kama viongozi wa serikali hatutaweza kuvivumilia vitendo vya namna hiyo tutapambanana kwa ajiri ya maslahi ya wakulima hawa.”
Akitoa taarifa rasmi, Mwenyekiti wa Ushirika Mkoa wa Lindi ameishukuru serikali kupitia wizara ya kilimo kwa fursa mbalimbali wanazozitoa kwa wakulima ili kuhakikisha kuwa wanawajengea mazingira rafiki ya kufanya shughuli zao.
“tunaishukuru serikali kwa mchango wao mkubwa wanaoendelea kuutoa katika sekta yetu ikiwemo utoaji wa pembejeo bure kwa wakulima wa korosho, kuongezwa kwa kodi za ushirika zinazochangia uendeshwaji wa shughuli za kiushirika, utoaji wa pembejeo za ufuta bure na uanzishwaji wa mfumo wa ununuzi kupitia stakabadhi ghalani.Licha ya hayo bado tuna ombi la kuingizwa katika mfumo wa ununuzi wa kupitia stakabadhi ghalani kwa zao la ufuta kama ilivyo kwa zao la korosho la ufuta ili kuchochea maendeleo ya uzalishaji wa zao hili na wakulima kiujumla” Ameeleza.
Kwa upande wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo {SIDO} Mkoa wa Lindi amewasisitiza wakulima kuendelea kuanzisha viwanda vidogo ili kuongeza thamani za mazao yao wanayoyazalisha na kuongeza kuwa kazi kubwa ya SIDO ni kuhudumia na kusimamia viwanda vidogo hivyo wataendelea kuwasogezea teknolojia na kuwaunganisha na Shirika la Viwango Tanzania {TBS} ili bidhaa zao ziweze kukaguliwa na kupatiwa nembo ya ubora.
Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Lindi limebeba ujumbe wa ‘Ushirika ni Maendeleo’ limeweza kuwakutanisha wana Ushirika na Vyama vya Msingi, Taasisi za kifedha na Bodi mbalimbali za mazao kwa lengo la kutoa elimu kuhusu ushirika, maonyesho ya bidhaa na huduma za wanaushirika sambamba na maonyesho ya bidhaa na huduma za wadau mbalimbali wa ushirika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.