Wakulima mkoani Lindi watakiwa kuandaa mashamba kwa ajili ya kupanda miche mipya ya mikorosho.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi amewataka wakulima kuandaa mashamba kwa ajili ya kupanda miche mipya ya mikorosho.
Mhe. Zambi aliyasema hayo wakati alipotembelea kukagua hali ya maandalizi ya vitalu vya miche mipya ya mikorosho katika wilaya za Liwale, Ruangwa na Nachingwea. Katika maeneo yote aliyopita alikuta vitalu vipo katika hatua mbalimbali ambapo maeneo mengine miche imeshatoka wakati maeneo mengine ikiwa bado.
“Miche hii inatolewa bure kwa wakulima hivyo wakulima wanapaswa kuanza kuandaa mashamba kwani hakuna mkulima atakayepewa miche kabla shamba lake halijakaguliwa na wataalam wa kilimo”, alisema Mhe. Zambi. Malengo ya Mkoa wa Lindi ni kuongeza uzalishaji wa zao la korosho katika miaka hii mitano ili mkoa ushike namba moja kiuzalishaji Tanzania.
Aidha, amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote za mkoa wa Lindi kuhakikisha wanazalisha miche ya kutosha ili kufikia malengo yaliyowekwa kwa kila wilaya. Kwa mkoa wa Lindi malengo yaliyowekwa ni kuzalisha miche mipya ya mikorosho 6,922,000.
Vilevile wakulima wametakiwa kutumia vizuri fedha wanazozipata kutokana na mauzo ya korosho katika kujiletea maendeleo. Mhe. Zambi amewasihi wa kulima kutumia fedha hizo katika kuboresha makazi, kununulia mahitaji ya watoto shuleni, kununua chakula cha kutosha na kufanya mambo mengine yenye tija katika kaya zao na jamii kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.