Wakulima wa korosho wahakikishiwa malipo yao
Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Japhet Justine amewahakikishiwa wakulima wa korosho kuwa watalipwa fedha zao.
Kauli hiyo ameitoa mkoani Lindi alipomtembele Mkuu wa Mkoa kwa lengo la kumueleza hatua ya malipo iliyofikiwa ambapo tayari TADB imeshalipa shilingi 3,184,179,98 kwa wakulima 3,592 wa mkoa wa Lindi ambao tayari wameshafanyiwa uhakiki.
“Niwahahakikishi wakulima wote wa korosho kuwa fedha zipo za kutosha na watalipwa fedha zao kama maelekezo ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa ya kumlipa mkulima shilingi 3,300 kwa kilo”, alisema Justine.
Justine alisema kuwa kabla ya malipo kufanyika ni lazima uhakiki ufanyike ili kujiridhisha kama kweli fedha zinazolipwa zinakwenda kwa mkulima wa korosho na si vinginevyo. Aidha, katika zoezi la uhakiki wamekutana na tatizo la utunzaji wa takwimu za wakulima katika baadhi ya vyama vikuu vya ushirika na vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) ambazo zinaonyesha taarifa za wakulima pamoja na taarifa zao za uzalishaji.
Pia amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwa maamuzi yaliyochukuliwa ya kuandaa fomu ambayo aitakuwa ni rahisi kwa vyama vikuu na AMCOS kujaza, itakayoonyesha taarifa zote muhimu za mkulima ambazo zitarahisisha kufanya zoezi la uhakiki pale utakapohitajika na kurahisisha malipo yaweze kufanyika kwa haraka zaidi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey W. Zambi amesema baada ya kuona zoezi la uhakiki linakwenda taratibu, ameunda timu shirikishi za uhakiki katika mkoa na wilaya ambazo zitashirikiana na TADB na bodi ya mazao mchanganyiko ili uhakiki uweze kufanyika kwa haraka sambamba na malipo ya wakulima.
Aidha, amewasihi wakulima kutoa ushirikiano kwa timu za uhakiki pale zitakapo pita kuahakiki, kwani lengo ni kujiridhisha kama anayelipwa ni mkulima sahihi na si vyinginevyo. Vilevile amewasihi wakulima kuwa watulivu kwa kuwa fedha za kuwalipa zipo na watalipwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.