Leo wanachama wa chama cha ushirika cha wakulima wa mwani wanaofanya shughuli ya ukulima wa mwani mji mdogo wa Kilwa Masoko wamepata faraja baada ya kutembelewa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega alipofanya ziara yake Mkoani Lindi.
Mhe. Naibu Waziri amekutana na wanachama hao alipotembelea kiwanda kidogo cha Kampuni ya Mwani Mariculture kilichopo Kilwa Masoko kinachochakata na kufungasha zao la mwani kabla ya kusafirisha kwenda sokoni.
Mhe. Naibu Waziri akiwa kwenye kiwanda hicho alizungumza na wakulima wa zao hilo linalolimwa kwa asilimia kubwa na wanawake, Wakulima walieleza changamoto wanazokabiliana nazo katika kilimo cha mwani ambazo ni pamoja na ugumu wa upatikanaji pembejeo ikiwemo kamba, taitai pamoja na bei ndogo ya Tsh. 500 kwa kilogramu 1 ya mwani.
Akiipongeza kampuni ya Mwani Mariculutre kwa kuendelea kununua mwani wa wakulima wa Kilwa Masoko, Mhe. Abdallah Ulega amewaomba wakulima hao kulima kwa wingi mwani aina ya cottonii ambao unahitajika kwa kiasi kikubwa sokoni na bei yake ni nzuri takribani Tsh. 1,500 kwa kilogramu moja huku akiwaahidi kuwaletea mbegu bora ya aina hiyo ya mwani.
Pamoja na ahadi za uwezeshwaji wa mbegu bora, Mhe. Abdallah Ulega amewaahidi wakulima hao kuwawezesha kamba pamoja na vichanja bora vya kuanikia mwani vyenye ukubwa mpaka mita 100 ili watunze ubora wa zao hilo kwa kutoanika chini.
Katika kuhakikisha ahadi hizo zinatekelezwa aliwaagiza viongozi na wataalam wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji alioambatana nao kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kukaa na viongozi wa Chama cha Wakulima wa mwani Kilwa Masoko ili kupitia nyaraka zao na kuanza mara moja utekelezaji wa kukiwezesha chama hicho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.