Wanafunzi kidato cha sita 2019 wapongezwa
Wanafunzi waliomaliza kidato cha sita 2019 wamepongezwa kwa kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa Lindi, Godfrey Zambi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya ufaulu wa wanafunzi waliofanya mitihani ya kitaifa ya kidato cha sita (6) 2019. Ambapo mkoa wa Lindi umeshika nafasi ya kwanza kitaifa kwa ufaulu mzuri na kufanikiwa kuondoa daraja la 0 na daraja la nne wapo wanafunzi 6 tu.
Zambi amesema ufaulu huu umeonyesha matokeo ya jitihada kubwa za viongozi, walimu, wadau, wazazi na wanafunzi katika mkoa wa Lindi zenye lengo la kuongeza ufaulu ikiwa ni pamoja na kuondoa daraja 0. Mkoa umekuwa na mikakati mbalimbali ya kunyanyua ufaulu ambayo imeainisha majukumu ya kila mhusika.
“Niwapongeze sana vijana waliomaliza kidato cha sita 2019 katika shule za mkoa wa Lindi kwa kupata matokeo mazuri katika mitihani yao ya mwisho”, alisema Zambi.
“Pia niwapongeze viongozi wote kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilaya, walimu, bodi za shule, wadau, wazazi/walezi kwa michango na juhudi za ufundishaji na usimamizi mlioufanya kuwezesha wanafunzi kufaulu vizuri na kuufanya mkoa wa Lindi kushika nafasi ya kwanza kitaifa”, aliongeza Zambi.
Aidha, viongozi, wadau, bodi/kamati za shule, walimu, wazazi/walezi wamehimizwa kuongeza juhudi hizi katika kusimamia utekelezaji wa mkakati wa mkoa wa kuongeza ufaulu. Vilevile, Mkuu wa Mkoa Zambi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa jitihada anazozifanya katika kuboresha miundombinu, kuajiri walimu, pamoja na kutoa fedha za elimu bure.
Naye Katibu Tawala Msaidizi – Elimu, Vicent Kayombo amesema kuwa matokeo hayo yameongeza ari ya ufundishaji kwa walimu na ufuatiliaji kwa viongozi kwenye utekelezaji wa mkakati wa mkoa wa kunyanyua elimu. Mkoa wa Lindi kwa matokeo ya mitihani ya kidato cha sita 2018 ulishika nafasi ya pili ukitanguliwa na mkoa wa Mtwara.
Mkoa umeshika nafasi ya kwanza kitaifa kwa kuwa na matokeo ya daraja la kwanza wanafunzi 228, daraja la pili 544, daraja la tatu 174 na daraja la nne 6, hivyo mkoa umefanikiwa kuondoa daraja sifuri. Kutokana na matokeo haya nguvu kubwa imeendelea kuwekwa kwa wanafunzi wa wanaofanya mitihani ya kitaifa mwaka huu ili na wao waweze kufanya vizuri.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.