Kumekuwepo na tatizo la baadhi ya wakazi hasa vijana kutumia muda wa kazi kwa kucheza pool table, kunywa pombe na kufanya shughuli ambazo zimekatazwa kufanyika muda wa kazi.
Akizungumza na wakazi wa mtaa wa Nanyanje na Jangwani, wakati alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi aliwataka wakazi hao na mkoa mzima kutumia muda wa kazi kwa kufanya kazi na si vinginevyo.
“Wakati nikiwa njiani nimekuta vijana wanacheza pool table na wengine nimewakamata, niwasihi wananchi wote wa mkoa wa Lindi kuhakikisha mnafanya kazi na si kukaa kwenye vijiwe vya pombe, bangi, pool table na vingine kama hivyo wakati wa muda wa kazi”, alisema Zambi.
‘Kutokana na hili, niwaagize watendaji wote wa Kata, Mitaa na Vijiji kuhakikisha wanasimamia maelekezo yanayotolewa na serikali likiwemo na hili la vijana kutocheza pool muda wa kazi, kwani kwa kutofanya hivyo watachukuliwa hatua’, aliongeza Zambi.
Aidha, Zambi aliwataka viongozi wa wilaya kuhakikisha wanawasimami watendaji walio chini yao ili nao wahakikishe maagizo na maelekezo yanayotolewa na viongozi yanatekelezwa.
Pia wamiliki wote wa pool table wametakiwa kuzingatia na kutekeleza maelekezo ambayo yanatolewa na viongozi, kwani kwa kutofanya hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga alisema kuwa maelekezo kuhusu agizo hilo walishayatoa sema kumekuwepo na baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakikaidi na pale ambapo wanakamatwa huchukuliwa hatua. Pia amemuhakikishia mkuu wa mkoa kuwa ataendelea kulisimamia agizo hilo huku akiwataka watendaji kutimiza wajibu wao wa kusimamia kwenye maeneo yao.
Kijana aliyekamatwa akicheza, Ismail Hassan ambaye ni mzaliwa wa mtaa wa Chikonji alisema kwa upande wake yeye hakujua kama kuna katazo lolote kwani walikuwa wakicheza pasipokuwa na katazo kutoka kwenye uongozi wa mtaa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.