Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amefanya ziara katika mkoa wa Lindi kwa lengo la kufanya thathmini ya utekelezaji wa zoezi la uandikishaji wa Anwani za Makazi katika mkoa wa Lindi, kupata changamoto na kutoa hamasa ya ushiriki wa wananchi katika zoezi hilo.
Akitoa taarifa ya mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga amesema “Kama mkoa tumeweza kufikia lengo kwa asilimia 98 ya uandikishaji huku kazi kubwa tuliyobakiwa nayo ni uwekaji wa nguzo katika mitaa mbalimbali ambapo hadi kufikia wiki ijayo tunatarajia kuikamilisha kazi hii. Laini pia kazi hii imesaidia mkoa kuimarisha uhusiano na ushirikiano na taasisi nyingine za mawasiliano kama TTCL na Posta”
Mhe. Ndemanga ameongeza kuwa kama mkoa umeweza kukumbana na changamoto mbalimbali wakati wa utekelezaji wa zoezi hili ikiwemo changamoto ya kimtandao iliyopelekea mfumo kutokua stable pamoja na kutopatikana kwa taarifa za wamiliki hasa wamiliki za ardhi.
Aidha, Mhe. Nape ametoa pongezi kwa uongozi wa Mkoa na Wananchi kwa ushirikiano walioutoa wakati wa utekelezaji wa zoezi hili na kupelekea Mkoa kuwa miongoni mwa Mikoa Kumi Bora katika utekelezaji wa zoezi hili na kuwataka viongozi kushirikisha wananchi katika utoaji wa majina ya barabara ikiwemo kutoa majina yatakayohifadhi historia ya maeneo husika.
“Tutumie mfumo huu kutunza historia ya maeneo yetu na hasa wanachi na viongozi kutoa majina ya mitaa na barabara yanayoendana na historia ya maeneo husika au majina ya viongozi wetu waasisi wa Taifa. Mfano kwa hapa Lindi mnaweza kutoa jina la barabara ya Tendaguru.
Waziri Nape pia amewataka wananchi kulinda miundombinu inayotumika katika zoezi hili ikiwemo nguzo ambazo zimetengenezwa kwa vyuma ili isije kuharibiwa na baadhi ya watu kwa maslahi yao binafsi kama matumizi ya biashara ya chuma chakavu.
Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikadi unaoendeshwa Kidijitali ni sehemu ya maandalizi ya Sensa ya Watu na unatarajiwa kukabidhiwa kwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ifikapo Mei 22, 2022.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.