Wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa wameeleza furaha yao kutokana na uwepo wa Kambi ya madaktari bingwa inayoendelea katika wilaya hiyo ambayo inatoa fursa za huduma za uchunguzi na matibabu ikiwemo na huduma za upasuaji bure.
Huduma hizo zinazohusisha uchunguzi na matibabu ya magonjwa kama Moyo, Mifupa, Figo, Magonjwa ya akina mama pamoja na huduma za upasuaji wa mgongo wazi na Kichwa maji {Hydrocephalus}, macho, afya ya watoto na huduma za afya ya Kinywa na Meno zinatolewa na Madaktari bingwa kutoka katika hospitali kubwa 8 ikiwemo Hospitali ya Rufaa Bugando, Hospitali ya Kanda ya Kusini, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine, Hospitali ya Mwananyamala, Nyangao, Ndanda na Hospitali ya Rufaa ya Taifa Muhimbili.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi Dkt. Kheri Kagya ameeleza kuwa lengo kuu la uwepo wa kambi hiyo ni kutoa huduma za kiuchunguzi na kitabibu kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi na maeneo jirani bure "Huduma hizi zinaendeshwa hapa kwa muda wa siku saba kuanzia tarehe 25 Novemba hadi tarehe 30, hii leo ni siku ya tatu, muitikio ni mkubwa, wananchi wamejitokeza kwa wingi kupata huduma za kichunguzi na matibabu na hadi kufikia leo tumeshahudumia wananchi takribani 930 tumshawafikia katika siku hii ya tatu. Katika huduma tunzotoa tunahusisha na matibabu ambapo kwa wagonjwa watakaohitaji kupatiwa dawa hapa watapata bure lakini pia kwa watakaohitajika kufanyiwa upasuaji pia watapata huduma hiyo bure"
Aidha, kambi hiyo sio tu imerahisha upatikanaji wa huduma za afya karibu na wananchi lakini pia unatarajia kutoa takwimu muhimu katika sekta ya afya kuhusu uwepo wa maradhi yanayoisumbua zaidi jamii kama anavyoeleza Mganga Mkuu wa Mkoa.
"Kupitia kambi hii tunatarajia sisi kama sekta ya afya kupata takwimu sahihi za magonjwa yapi yanayoisumbua jamii yetu kwa sasa mfano hapa tangu tumeanza kambi hii tumeona magonjwa ya macho kama mtoto wa jicho, trakoma na presha ya jicho ni maradhi ambayo yanawasumbua wananchi wengi wanaofika hapa, eneo la meno, magonjwa ya akina mama hivyo hapa tunaona ni maeneo gani yanapaswa kuwekewa nguvu zaidi ili afya za wananchi ziwe katika mikono salama" ameongeza.
Veronica Juma ni mama ambaye mtoto wake amepata huduma ya matibabu ya jicho na hapa anatuelezea namna ambavyo amepata huduma hiyo "Mtoto wangu alitokwa na kipele kidogo pembeni ya jicho, nilivyosikia kuhusu uwepo wa madaktari bingwa nilijitokeza mwanangu akapata uchunguzi akaandikiwa aje kufanyiwa upasuaji, kwakweli tumepokelewa vizuri sana na tumehudumiwa vizuri. Napenda tu kuchukua nafasi hii kumshukuru Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan na Mbunge wetu kwa kutuletea huduma hizi bure hili sio jambo dogo wametufikiria vizuri sana na hapa sijatozwa hata Shilingi elfu mbili ya kununulia kiwembe, nawashukuru pia na madaktari na wauguzi wote waliotuhudumia"
Naye, Mzee Salumu Abdallah Masudi ameeleza shukrani zake baad ya kupatiwa huduma ya upasuaji wa tatizo la Ngirimaji {Busha} lililokuwa linamsumbua "Nashukuru Mungu upasuaji wangu haujasumbua kabisa madaktari na wauguzi wamenihudumia vizuri na kwa upendo, mwanzoni nilishindwa kumudu gharama za upasuaji, nilivyosikia habari za huduma za afya za kibingwa bure nikajitokeza na nashukuru kwakweli huduma zimekuwa za kuridhisha na ni bure kama walivyosemA hatujachangia chochote"
Kambi ya Madaktari Bingwa wilayani Ruangwa inatarajiwa kudumu kwa takribani siku saba (7) na inatarajiwa kutoa huduma za uchunguzi, huduma za matibabu kama dawa pamoja na huduma za upsuji bure kwa wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.