Wananchi wa Mkoa wa Lindi wametakiwa kujitokeza na kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka huu ifikapo tarehe 23, Agosti.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Ndg. Kasper Mmuya wakati wa ziara yake yenye lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa operesheni ya anuani za makazi katika mkoa wa Lindi.
“Kuna dhana nyingi za tofauti kuhusiana na kuhesabiwa kwa watu lakini tujitahidi kuwaelewesha wananchi wetu kuhusu umuhimu wa Sensa kama tulivyofanya katika anuani za makazi, kwamba zoezi hili ni kwa maendeleo yetu sisi wenyewe na kusaidia serikali katika utoaji wa huduma muhimu na za kijamii kwa wananchi kama ujenzi wa vituo za afya na elimu” Ndg. Mmuya.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu ametoa pongezi kwa Mkoa kwa utekelezaji wa jumla wa operesheni ya anuani za makazi ambazo zimepelekea zoezi hilo kufanikiwa kimkoa kwa 131% licha ya changamoto za kijiografia zilizopo.
“Bado kuna malalamiko kutoka kwa wananchi wa maeneo mbalimbali kwamba nyumba zao bado hazijatambulika, nitoe rai wafike kwanza katika ofisi za mtendaji wa kata katika maeneo yao ili kujihakikisha kama nyumba zao kweli hazijatambulika, lakini pia niwakumbushe wananchi wote kuwa jukumu la kutoa taarifa rasmi za makazi yao, uwekaji wa vibao vyenye namba ikiwemo na kutumia na kutunza miundombinu ya mfumo wa anuani za makazi ni wajibu wao”ameongeza.
Vilevile, Naibu Katibu Mkuu amewataka TARURA kuhakikisha wanatambua barabara zao pamoja na kuziwekea nguzo na alama za barabarani ambazo zitaeleweka kwa watumiaji wote wa barabara hizo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.