Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi,Ndugu Ngusa Samike ametoa rai kwa wananchi wa mkoa wa Lindi kulinda na kutumia miundombinu ya barabara ikiwemo madaraja ipasavyo ili kujiepushia adha ya kukosekana kwa huduma ya usafiri katika maeneo yao.
Katibu Tawala ametoa rai hiyo alipotembelea ukarabati wa daraja lililojengwa kwa kutumia nyenzo za vyuma lililopo Kijiji cha Nng’uni, wilaya ya Ruangwa ambalo lilivunjika baada ya watu wasio waaminifu kufungua na kuiba baadhi ya vyuma vya maungio ya daraja hilo na kupelekea daraja hilo kushindwa kuhimili roli ambalo lilizidisha uzito wa mzigo unaotakiwa kupitishwa katika daraja hilo.
Pia, Ndg. Ngusa ameitaka Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini {TARURA} kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya miundombinu ya barabara na kuongeza kuwa itawasaidia kuepuka kuzidisha uzito wa mizigo ambayo itashindwa kustahimiliwa na uwezo wa madaraja yanayojengwa.
“Tunapojenga madaraja kama haya tunatumia fedha nyingi kuyajenga, na kwa materials yaliyotumika hapo ni vyuma hivyo inawavutia watu waharibifu kuyaharibu kwa manufaa yao na kuhatarisha Maisha ya watu wengine kama ambavyo ajari iliyopelekea daraja hili kuvunjika ilivyotokea. Hivyo niwatake tu wananchi kuwa walinzi kwa wao kwa wao ili kukomesha vitendo hivi athari ya moja wapo imewakuta hapa pamekosekana mawasiliano kwa muda takribani miezi miwili, na TARURA pia niwatake muwe mnatoa elimu kwa wananchi na sio kuwajengea tu na kuwaacha waendelee na matumizi wenyewe na muwashirikishe wananchi wa pembezoni kuzingatia uzito wa magari yanayopita hapa ili tuendeleze uimara wa daraja hili”Amesema.
Mhandisi Filbert Mpalasinge, Meneja wa TARURA Mkoa wa Lindi amesema kuwa wana jukumu la kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika madaraja ili kujua kama kuna uchakavu ama upotevu wa vifaa ili waweze kufanya ukarabati kwa mapema na kuepuka athari kama zilizojitokeza.
“Katika ulindaji wa madaraja haya hasa ya chuma tumeanza kufanya ushirikishaji wa wananchi na viongozi katika ngazi zote ili kuwa na ulinzi shirikishi kuweza kuzuia vitendo vya ubadhilifu katika miundombinu yetu,lakini pia sisi tuna jukumu la kukagua mara kwa mara ili kuona kama kuna vifaa vimeshaanza kuibiwa tuweze kuvirejesha mapema, lakini pia kuna suala la kudhibiti uzito madaraja yetu yanabeba uzito usiozidi tani 15 lakini hap ahata lori lililosababisha ajari lilibeba mchanga wenye tani zaidi ya 25 hivyo nitoe rai kwa wananchi kufuata maelekezo na utaratibu ikiwemo kuzingatia vibao vilivyopo barabarani’’
Athuman Bakuli, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nng’uni ameishukuru TARURA kwa kuharakisha ukarabati wa daraja hilo na kurejesha huduma ya usafiri kwa wananchi “Uwepo wa daraja hili ni muhimu sana kwa wananchi wanaoishi hapa na wale wa ng'ambo ya mto huu wa Lukuledi ukizingatia daraja hili ndilo linalotenganisha mkoa wa Lindi na Mtwara hususani katika Wilaya za Ruangwa na Masasi hivyo tunaishukuru sana serikali na wakala wa barabara kwa kuona uzito wa kurejesha daraja hili hapa, sisi hapa tunategemeana watu wanaotoka ng’ambo wanakuja kulima huku kwetu na sisi kule tunategemea sana kupata maji na ndio njia kuu ya wananchi kuvuka Kwenda Ndanda hospitali’’
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.