Wananchi wa Kijiji cha Milola, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi wameishukuru serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kujengewa daraja ambalo limekuwa kiunganishi na kichochezi cha mahusiano mazuri yaliyopo kati yao na wananchi wengine waishio maeneo ya jirani ikiwemo Nangaru na Kikomolela.
Hayo yamesemwa wakati wa ziara ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Bwana Ngusa Samike yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya Barabara inayotekelezwa na kusimamiwa na TARURA katika mkoa wa Lindi.
Awali akitoa maelezo ya mradi huo Meneja wa TARURA wilaya ya Lindi Mhandisi Dawson Paschal amesema “ ujenzi wa daraja la Milola umegharimu kiasi cha Milioni 300 ambapo ulihusisha ujenzi wa daraja kwa na ujenzi wa vented drift katika barabara ya Milola- Nangaru, mradi huu umetekelezwa na Mkandarasi M/s Construction Company Limited ambapo mkataba wake ulianza tarehe 8 Agosti na kukamilika tarehe 8 Disemba 2022 na utekelezaji wake umekamilika kwa asilimia 100’’
Selemani Yusuph Namtumba,Mkazi wa Milola ameeleza shukrani zake kwa serikali kwa ujenzi wa daraja la Milola na ukarabati wa barabara unaoendelea “ Tunashukuru sana kwa ujenzi huu unaoendelea hasa kwa barabara hii ya Milola-Nangaru kwa maana ilikua ni kikwazo kidogo kwa shughuli zetu tunazozifanya kila siku lakini kwa sasa tuna matumaini makubwa mno, kabla ya ujenzi huu hali ya usafiri ilikua ni mbaya mno hatukuweza kupita eneo lile hata kwa baiskeri lakini sasa tunapita na usafiri wowote ule hii imefanya kuimarika hata kwa ufanyaji wetu wa baishara na usafirishaji wa bidhaa zetu kwa ujumla”
Naye, Karim Mmaka ameipongeza TARURA kwa kazi wanazozifanya hasa ujenzi wa barabara na daraja katika maeneo ya Milola na kuongeza kuwa ujenzi huo unaenda kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa katika maeneo yao “ Nipende kuchukua nafasi hii kuipongeza tu TARURA na serikali kwa ujumla kwa kazi kubwa wanayoifanya, daraja hili linaenda kupunguza njia ya mzunguko tuliyokuwa tunapita mwanzo kutoka hapa Milola ili tuweze kufika sehemu tuliyokuwa tunakusudia Kwenda, hili daraja limekuwa mkombozi kwetu kwasababu linaenda kupunguza vifo vya watu hasa wanafunzi wanaotoka ng’ambo ya pili kuja huku kuja shuleni katika majira ya masika”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.