Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi katika Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa amewaasa wananchi wa Mkoa wa Lindi kuenzi maisha ya Mashujaa waliotangulia mbele ya haki kwa kuwa wazalendo.
Mhe. Ndemanga ameyasema hayo jana katika viwanja vya mpira wa basketi vilivyopo jirani na bwalo la Polisi alipokuwa akizungumza na wananchi walioshiriki Maadhimisho hayo ambayo Kimkoa yamefanyika Manispaa ya Lindi.
Mhe. Ndemanga amesema kuwa katika kuwaenzi Mashujaa wetu tuendeleze umoja, mshikamano na uzalendo kwa kujitolea kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na maendeleo kama vile usafi wa mazingira kwenye maeneo ya jamii.
Kwa upande wao Viongozi wa dini wakisoma sala na dua ya kuwaombea Mashujaa wamesema kuwa amani ya Taifa la Tanzania imeendelea kuimarika kutokana na maombi na sala za Mashujaa waliotangulia mbele za haki.
Aidha, Viongozi wa dini wamesisitiza kuwa wananchi wote wanapaswa kuitunza tunu ya amani kwa kuendelea kuitunza vyema nchi ya Tanzania pamoja na kuwaombea Viongozi wa Taifa wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Mkoa wa Lindi yamefanyika mapema jana Jumanne, tarehe 25 Julai 2023 ambapo awali wananchi walishiriki shughuli ya usafi wa mazingira katika soko kuu la Manispaa ya Lindi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.