Wananchi wa Kitongoji cha Nyengedi, Halmashauri ya Mtama, Wilaya ya Lindi wameishukuru serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini {TARURA} kwa kuwajengea kivuko cha watembea kwa miguu ambacho kimekuwa suluhisho la usafirishaji wa watu pamoja na kuimarisha mawasiliano kati yao na watu waishio ng’ambo ya Mto Lukuledi.
Hayo yamejiri wakati wa ziara ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Ndg. Ngusa Samike yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya barabara inayotekelezwa na TARURA katika mkoa wa Lindi ambapo licha ya kupongeza kazi zinazofanywa na TARURA kuunganisha mtandao wa barabara katika mkoa wa Lindi amewataka pia wananchi kutunza miundombinu inayotumika ili iweze kuwanufaisha kwa muda mrefu.
“ Wananchi walishalalamika sana kuhusu eneo hili kuwa na usumbufu katika kuvuka hususani kipindi cha mvua ambapo huu mto huwa unafurika,TARURA wameshatimiza jukumu lao sasa ni jukumu la wananchi kuhakikisha daraja hili linatunza na hili tutawaandikia na barua viongozi wa kijiji wawe wanakagua na kuwaeleza wananchi kuwa walinzi wa miundombinu iliyopo hapa kama linavyoonekana daraja hili limetengenezwa kwa vyuma sasa wasianze kuja kukata na kubomoa hiki kivuko kitapoteza ubora wake na matokeo yake tutarudi kulekule kwenye kero, hivyo kuanzia ngazi ya Kijiji inabidi wajipange kusimamia na kulilinda daraja hili” amesema Katibu Tawala Mkoa.
Meneja wa TARURA wilaya ya Lindi, Mhandisi Dawson Paschal ameeleza kuwa kivuko cha watembea kwa miguu kimeunganisha vijiji viwili vya Kitongoji cha Nyengedi ambavyo ni Nyengedi A na Mitandi ambavyo kwa muda mrefu ifikapo nyakati za masika vimekuwa vikikosa mawasiliano kutokana na kufurika kwa Mto Lukuledi.
“Kivuko hiki kimejengwa kupitia fedha za mfuko wa barabara yaani Road Fund baada ya wananchi kuleta kero yao ndipo tukafanya usanifu wa daraja hili na kuanza utekelezaji, daraja hili lina urefu wa mita 67 na limegharimu kiasi cha milioni 123 na ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100 hivyo kimeshaanza kutumika na wananchi, ujenzi wa daraja kama hili pia kwa mwaka huu unatekelezwa Mchinga 1, na tuna mpango wa kuendelea kujenga madaraja mengine mawili, moja litakuwepo pia Mchinga katika Kijiji cha Sinde na la pili litakuwepo hapa Mtama katika Kijiji cha Mtualonga” Mhandisi Dawson.
Amina Hassani, mkazi wa Kijiji cha Nyengedi A ameeleza athari zilizotokea kabla ya uwepo wa kivuko hiko katika kitongoji chao “awali tulikua tunatumia kivuko cha madumu na kiukweli kulikua na athari nyingi sana, watu wametumbukia sana mtoni wamezama wengine wamechukuliwa na Mamba, wengine walifanikiwa kuokolewa. Nyakati za mvua hapa kulikuwa hakuna mawasiliano wa ng’ambo walikuwa hawawezi kuvuka hata ikitokea msiba na wanafunzi wanakaa majumbani hadi maji yapungue ila kwa sasa tunashukuru hapa maji hata yajae vipi tuna uwezo wa Kwenda ng’ambo muda wowote tunaoutaka hata iwe usiku’’
Haroon Shomali, mkazi wa Nyengedi ameishukuru serikali kwa kuwajengea kivuko hiko kwani kimewapa uhakika wa kuendelea na shughuli zao hasa za kilimo “daraja hili limeleta chachu kwa kweli na wananchi tunashukuru sana kwa kuwekewa hili daraja, limetuhamasisha sana kuendelea na shughuli zetu ukizingatia asilimia kubwa ya wakazi wa Nyengedi wana mashamba yao ng’ambo ya huu mto Lukuledi na kwa sasa tunasafirisha hadi mazao yetu kwa kupitia kivuko hiki.’’
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini {TARURA} wilaya ya Lindi ina jumla ya mtandao wa barabara zenye urefu wa km 563.10 kwa upande wa Halmashauri ya Mtama ambazo zina mgawanyo wa lami, changarawe na udongo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.