WANANCHI WAASWA KUSHIRIKI ZOEZI LA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA. UZINDUZI 2024
Posted on: August 2nd, 2024
WANANCHI WAASWA KUSHIRIKI ZOEZI LA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA.
Wananchi watakiwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu ili kupata nafasi ya kuchagua viongozi bora watakaoleta chachu ya maendeleo katika sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Nanenane Kanda ya Kusini yanayofanyika katika Viwanja vya Nanenane Ngongo, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi.
"Ni matumaini yangu kuwa wananchi wote wenye sifa za kupiga kura watajitokeza katika zoezi zima la uboreshaji wa daftari la wapiga kura pamoja na kushikiri katika zoezi la kupiga kura ili kuchagua viongozi wenye sifa watakaochochea maendeleo na kuchaguza katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji, kupata viongozi bora kunategemea ushiriki wetu sote katika uchaguzi" Mhe. Telack
Aidha, Mkuu wa Mkoa ameendelea kusisitiza kuwa kila kaya kuwa na angalau heka tatu watakazotumia katika uzalishaji wa mazao ya kilimo ya chakula na biashara ili kuwa na uhakika wa chakula katika familia.
"Niendelee kusisitiza kuwa na ekari angalau tatu tutakazotumia kupanda mazao kama mihogo, mahindi, mtama na mazao ya bustani kama mbogamboga na matunda ili tuwe na uhakika wa chakula katika familia zetu na fedha tutakayopata kutoka katika mazao yetu ya biashara tuende tukatumie katika shughuli nyingine za kimaendeleo kama kuboresha makazi yetu, uwekezaji katika biashara na kusomesha watoto wetu" ameongeza.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Mwanahamis Munkunda ameeleza mikakati ya uboreshaji wa kilimo iliyofanywa na serikali katika kuhakikisha wanafanyaa uzalishaji wenye tija katika kilimo ikiwemo utoaji wa pembejeo za kilimo bure na ugawaji wa vipimaudongo katika Halmashauri ili kuwawezesha wakulima kufahamu aina za mazao wanazoweza kuzalisha katika maeneo yao kulingana na aina ya udongo.
Maadhimisho ya Maonyesho ya Nanenane yamefunguliwa leo rasmi yakiwa na kauli mbiu isemayo "Chagua Viongozi wa Serikali za Mitaa kwaMaendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi"