Wananchi waaswa kutoa taarifa za moto
Wananchi wa mkoa wa Lindi wametakiwa kutoa taarifa sahihi za moto na majanga mbalimbali pale yanapojitokeza.
Hayo yamesemwa na mkuu wa mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi wakati alipotembelea mtaa wa mnazimmoja kuangalia madhara yaliyotokea kutokana na moto ulioteketeza baa inayofahamika kwa jina la SAKINA na nyumba mbili za wananchi.
Mhe. Zambi licha ya kutoa pole kwa waathirika wa janga hilo, amewataka wananchi kujenga tabia ya utoaji taarifa sahihi kwa wakati katika maeneo husika hasa kwa jeshi la zimamoto na kushirikiana na waathirika kuuzima moto.
“Kumekuwepo na tatizo la baadhi ya watu pale majanga yanapotokea kukimbilia kuiba vitu badala ya kusaidia kuokoa mali, tabia hii ni mbaya katika jamii kwani tunapaswa kuwa na huruma kwa wenzetu waliopatwa na matatizo, na pale mnapomuona mtu anafanya vitendo kama hivyo mnatakiwa kumfikisha kwenye vyombo vya sheria,” alisema Mhe. Zambi.
Aidha, Mhe. Zambi amemuagiza mkuu wa wilaya ya Lindi kuhakikisha inafanyika tathmini ya hasara iliyosababishwa na moto huo na kuona ni namna gani wanaweza kuzisaidia familia ambazo zimepoteza chakula na sehemu zao za makazi.
Kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa, INSP.Peter N Mziwanda alisema kuwa walipokea taarifa za awali kuwa kuna gari linaungua maneneo ya mnazi mmoja na alituma kikosi chake lakini baadae akapata taarifa kuwa baa ndio inaungua na imeezekwa kwa makuti ndipo akatuma kikosi kingine. INSP. Mziwanda amewasihi wananchi kuhakikisha wanafikisha taarifa zilizo sahihi na kwa wakati pale majanga yanapotokea. Pia wananchi wamaaswa kuhakikisha wanauteketeza moto na kuhakikisha umezimika pindi wanapomaliza matumizi yake.
Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo Ndg. Habib Fadhili amesema chanzo cha moto huo ni upepo uliopeperusha moto uliokuwa unatumika kuchomea taka baada ya usafi kufanyika na kupelekwa kwenye tawi la mnazi ambalo lilikatika na kuangukia kwenye paa la baa hiyo ambayo imeezekwa kwa makuti. Tatizo kubwa lililojitokeza ni baadhi ya watu kukimbilia kuiba vitu na hela kaunta badala ya kusaidia kuokoa mali.
Moto huo baada ya kuunguza baa pia ulirukia kwenye nyumba nyingine mbili ambazo nazo ziliteketea zikiwa na vitanda, magunia 10 ya mpunga, magunia ya mahindi,fedha taslimu sh.laki mbili na vyombo vingine vya ndani.
Naye mmliki wa baa,Bi.Sakina amesema moto huo umemsababishia hasara ya vifaa vya mziki kama spika, friji mbili zilizokuwa na vinywaji, mashine na upotevu wa fedha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.