Wananchi watakiwa kulima alizeti
Wananchi wa kijiji cha Mchinga II na wilaya ya Lindi wametakiwa kulima alizeti kwa wingi kwa kuwa soko la uhakika lipo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi wakati alipotembelea kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti kinachomilikiwa na kampuni ya Kilimo Timilifu (KT) ambacho kimejengwa katika kijiji cha Mchinga II wilayani Lindi.
Mhe. Zambi amesema ujenzi wa kiwanda hicho kunatoa fursa kwa wananchi kunufaika kupitia kilimo cha alizeti kwa kuwa soko la uhakika lipo. Kinachotakiwa ni wananchi kuwatumia KT na wataalam wa kilimo ili wawasaidie namna bora za kilimo hicho.
“Viongozi na wataalam wa kilimo ni lazima muanze sasa kuwaelimisha wananchi njia sahihi za kilimo cha alizeti na kuwahimiza waanzishe mashamba kwa kuwa soko lipo”, alisema Zambi.
Pia amewasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki mafunzo yanayotolewa na kampuni KT ambao licha ya kutoa elimu ya kilimo cha alizeti kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira, wanatoa elimu ya kilimo cha mbogamboga na ufugaji wa kuku. Hii ni kutokana na taarifa alizopewa kuwa wananchi hasa katika eneo la mradi kutojitokeza kikamilifu katika kujifunza.
Aidha, ameipongeza kampuni kwa uamuzi wake wa kuja kuwekeza kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti katika kijiji cha Mchinga II wilayani Lindi. Uwepo wa kiwanda hicho licha ya kutoa ajira kwa wananchi pia kitanunua alizeti kwa wakulima, kununua kuku kutoka kwa wafugaji kwa ajili ya kuchinjwa katika machinjio iliyojengwa.
Akielezea shughuli za kampuni Katibu wa Kampuni, Mwassa Jingi amesema kampuni hiyo haina mmiliki bali inaongozwa na menejimenti kwa niaba ya wananchi na hupata msaada kutoka kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kukamilisha mradi ili waweze kuendesha shughuli zao wenyewe.
Jingi amemuomba Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine kuendelea kuwahamasisha wananchi kwenda kujifunza kuhusu kilimo hifadhi na kulima alizeti kwa wingi. Hii itawezesha kiwanda hicho chenye mahitaji ya tani 250 kwa mwaka kufanya kazi mwaka mzima kwa kuwa na uhakika wa kupata malighafi za kutosha kwani wao hawatalima alizeti badala yake watategemea kupata kutoka kwa wananchi.
Pia amemuomba kupitia kwa maafisa maendeleo ya jamii na maafisa mifugo kuanza kuwahamasisha wananchi kujiandaa na ufugaji wa kuku ambao vifaranga vyake vitakuwa vikizalishwa na kituo cha KT ambavyo vinatarajiwa kati ya Octoba-Novemba, 2019 vitaanza kutoka.
Vilevile ameomba wataalam wa halmashauri kutoa ushirikiano pale taaluma zao zitakapohitajika kwani kwa udogo wa kampuni haitaweza kuajiri watu wote.
Naye mkuu wa wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga amesema wilaya tayari imeshapata wakulima zaidi ya 4,000 ambao itawatambua kwa kujua ukubwa wa mashamba waliyonayo. Pia kulikuwa na changamoto ya upatikanaji wa mbegu lakini kwa kushirikiana na Aghakhan Foundation na mradi wa Tilage watasambaza mbegu hizo za alizeti. Hivyo KT kwa kushirikiana na wataalam watasaidia kuwaongoza wananchi kuhusu namna bora za kilimo cha alizeti.
Mtendaji Mkuu wa kampuni ya KT, Timoth Tanner licha ya kumshukuru mkuu wa mkoa kwa kutembelea mradi, amesema nia ya mradi ni kuwasaidia wananchi wa hali ya chini kuondokana na umaskini kupitia kilimo hivyo shughuli wanazopanga kufanya zinahitaji ushiriki wa wananchi kikamilifu.
Ahmed Selemani, mwenyekiti wa kitongoji cha kijiji cha Mchinga II ameshukuru kwa ujenzi wa kiwanda kwani wananchi watapata ajira na sehemu ya kuuzia alizeti watakazokuwa wanalima. Pia wananchi watanufaika na elimu ya kilimo hifadhi, kilimo cha mbogamboga na ufugaji wa kuku ambapo machinjio yake itakuwa kiwandani.
Katika ziara hiyo mkuu wa mkoa Zambi alitembelea bustani inayotumika kufundishia kilimo cha mbogamboga na kukutana na akina mama wanaofundishwa, alitembelea shamba na kuona eneo lililolimwa kwa kuzingatia kilimo hifadhi, eneo la kiwanda cha alizeti ambacho kipo tayari na machinjio ya kuku ambayo ipo katika hatua za umaliziaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.