Wananchi watakiwa kutunza na kuhifadhi mazingira
Wananchi wa Mkoa wa Lindi wametakiwa kuhakikisha wanatunza na kuhifadhi mazingira ili yawe endelevu kwa vizazi vijavyo.
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Ramadhani Kaswa ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi katika maadhimisho ya siku ya mazingira duniani ambayo kimkoa ilifanyika katika kijiji cha Nanjilinji wilayani Kilwa.
Kaswa alisema kuwa lipo tatizo la uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli za kibinadamu ambazo ni pamoja na uchomaji misitu, kilimo cha kuhamahama, utupaji taka ngumu hovyo, uharibifu wa vyanzo vya maji na uchomaji mkaa hovyo.
Pia alizitaja athari zinazotokana na shughuli hizi za kibinadamu kuwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, kupungua na kunyeesha kwa mvua bila mpangilio na kusababisha mafuriko, kutokea kwa ukame, na kuongezeka kwa magonjwa ya mlipuko mfano kipindupindu.
“Hivyo niwasihi wananchi wa mkoa wa Lindi kuhakikisha wanatunza na kuifadhi mazingira ikiwa ni pamoja kuacha kuchoma mkaa bila kufuata taratibu na kuanza kutumia nishati mbadala”, alisema Kaswa.
Vilevile wananchi wametakiwa kuhakikisha wanafanya usafi wa mazingira na kuzingatia agizo la Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli la usafi wa kila jumamosi ya mwisho wa mwezi.
Aidha, Kaswa amewapongeza wananchi wa Nanjilinji kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika uhifadhi wa mazingira ambapo kutokana na uhifandhi huo kijiji kimeweza kuanzisha miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa gesti ambayo itasaidia kuongeza mapato.
Pia amelipongeza shirika lisilo la kiserikali la kuhifadhi Mpingo na Maendeleo (Mpingo Conservation and Development) kwa kupata tuzo ya Rais ya uhifadhi bora wa mazingira kitaifa na kukifanya kijiji cha Nanjilinji kutambulika kitaifa na kimataifa.
Kauli Mbiu ya Siku ya Mazingira Duniani kimataifa kwa mwaka huu ni “Beat Plastic Pollution”. Ujumbe huu utuhimiza sisi wote kwa pamoja kuungana katika kupambana na changamoto ya uchafuzi wa mazingira utokanao na plastiki. Hivyo kauli mbiu ya siku ya Mazingira Kitaifa mwaka 2018 ni “MKAA NI GHARAMA: TUMIA NISHATI MBADALA”.
Maudhui ya ujumbe huu Kitaifa unalenga kuelimisha na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kwa wananchi ili kukabiliana na changamoto ya ukataji wa miti nchini. Aidha, ujumbe huu unalenga kuonesha madhara ya matumizi ya mkaa kimazingira, kiuchumi, kiafya na kijamii.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Ngubiagai kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi alisema kuwa Wilaya ya Kilwa inajitahidi sana katika kusimamia utunzwaji na uhifadhi wa mazingira. Aidha, zoezi la upandaji miti limekuwa likifanyika kilwa mwaka na wananchi mara kwa mara hukumbushwa suala la usafi wa mazingira ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyoo.
Kaimu Afisa Mazingira Mkoa, Jumbe Kawambwa alielezea baadhi ya malengo ya kuadhimisha siku ya Mazingira Duniani kuwa ni Kuongeza uelewa wa jamii juu ya umuhimu wa mazingira mazuri kwa maisha ya viumbe na maendeleo, Kutatua baadhi ya matatizo katika mazingira kwa kutekeleza shughuli rafiki na mazingira na Kuelemisha umma juu ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira kuwa ni wajibu wa kila mmoja, si serikali, vyombo vya habari, taasisi za serikali au zisizo za Serikali, kila mmoja wetu anawajibika kuyatunza Mazingira.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Nachinjili A aliesema kuwa wananchi wanatambua umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kwani baadhi yao wanategemea misitu kama njia ya kupatia kipato. Pia alieleza kuwa kijiji kinaendelea na upandaji miti mipya huku wananchi wakihamasishwa na wao kuwa na misitu yao.
Kabla ya kuongea na wananchi, Kaswa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa aliweka jiwe la msingi la kiwanda cha kupasua mbao kinachomilikiwa na Sound & Fair Industry, pia alizindua nyumba ya kulala wageni inayomilikiwa na serikali ya kijiji cha Nanjilinji A.
Maadhimisho haya yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na taasisi binafsi pamoja na wananchi wa Kijiji cha Nanjilinji A na Kijiji cha Nanjilinji B.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.