Hayo yameelezwa asubuhi ya leo na mgeni rasmi Mhe. Shaibu Ndemanga Mkuu wa Wilaya ya Lindi akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi katika sherehe za ufunguzi wa maadhimisho ya kitaifa ya siku ya UKIMWI duniani zilizofanyika katika kiwanja cha michezo cha Ilulu kilichopo Manispaa ya Lindi.
Akizungumza mbele ya wananchi waliohudhuria sherehe hizo, Mhe. Ndemanga amesema kuwa wanaume wengi wamekuwa na mwitikio mdogo wa kupima VVU ukilinganisha na wanawake ambapo kwa uwiano inaonyesha kuwepo kwa kiwango cha chini cha upimaji kwa 45.3% ukilinganisha na 55.9% kwa upande wa wanawake. Mhe. Ndemanga amebainisha kuwa imegundulika wanaume wengi hawajitokezi kupima kwa sababu wanatumia majibu ya wenza wao kuwa ni vipimo vyao jambo ambalo linarudisha nyuma jitihada za kupambana na UKIMWI.
“Wanaume walio wengi wana mtizamo hasi wa kutafsiri majibu ya kipimo cha VVU cha wenza kwamba ndio majibu yao. Kiafya hali hii ni hatari sio tu kwa mtu binafsi bali pia kwa familia, kaya na Taifa kwa ujumla. Pia inadhoofisha juhudi za Serikali na wadu wa mwitikio wa VVU na UKIMWI nchini kufikia malengo ya kitaifa ya 95-95-95 ifikapo 2025 na hatimaye sifuri tatu mwaka 2030”.
Pamoja na mafanikio makubwa katika kupunguza maambukizi ya VVU ambapo kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2016/2017 kuonesha kushuka kwa kiwango cha maambukizi kutoka asilimia 7 mwaka 2003/2004 mpaka kufikia asilimia 4.8, Mhe. Ndemanga amewataka wanaume kujitokeza na kupima ili kujua hali ya afya zao jambo ambalo litawasaidia wao wenyewe, familia na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Dkt. Bora Haule akiwasilisha salam za mkoa amesema kuwa mkoa wa Lindi unaendelea na jitihada za mapambano ya VVU na UKIMWI, jitihada ambazo zimepelekea kushuka kwa maambukizi mpaka kufikia asilimia 0.3 kwa takwimu za mwaka 2016/17. Kiwango hicho cha maambukizi ambacho ni cha chini zaidi ukilinganisha na kiwango cha taifa cha asilimia 4.7, Dkt. Bora ameongeza kuwa katika utekelezaji wa malengo ya 95,95,95 Mkoa wa Lindi umefikia asilimia 92 ya wananchi wanaotambua hali zao za maambukizi VVU baada ya kupimwa, asilimia 98 kati ya waliogundulika kuwa na VVU wanatumia dawa, asilimia 95 kati ya watu wanaoishi na VVU ambao wanaotumia dawa za ARV wamefanikiwa kufubaza VVU.
Akitoa salam za Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Mkurugenzi wa taasisi hiyo Dkt. Leonard Maboko akiwahamasisha wananchi kupima magonjwa mbalimbali ikiwemo homa ya ini, kifua kikuu, kansa ya kizazi, UKIMWI na kupata chanjo ya UVIKO, amesema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Imarisha usawa” inalenga kuyafikia makundi ambayo yameachwa nyuma ikiwemo makundi ya watoto na maeneo ambayo yanafikika kwa shida. Dkt, Maboko ameongeza kuwa kwa sasa kila mwaka kuna maambukizi mapya 54,000 huku malengo mpaka kufikia 2030 inatakiwa kusiwe na maambukizi mapya wala vifo vitokanavyo na UKIMWI. Kwa mujibu wa takwimu zinaonesha kuwa kundi la vijana kati ya miaka 15-24 ndiyo linaathirika sana na maambukizi mapya huku wasichana wadogo wakiongoza kwa asilimia 80.
“Haya maambukizi mapya, ukilichukua lile kundi la vijana wenyewe, asilimia 80 ya wale vijana ni mabinti wenye umri huu wa miaka 15-24, hivyo tuna kazi kubwa ya kufanya kuwaondoa katika hatari mabinti, hata vijana wa kiume.” Amesema Dkt. Maboko.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.