Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amewataka wazazi wa Lindi kuhakikisha wanawasomesha watoto wao.
Mhe. Telack ameyasema hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayofanyika kila mwaka ifikapo tarehe 8, Machi ambapo katika Mkoa wa Lindi maadhimisho hayo yamefanyika katika wilaya ya Nachingwea, ambapo Mhe. Telack amese,a kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hasssan ameboresha huduma za elimu kwa kiwango kikubwa hivyo wazazi wawajibike kusomesha watoto wao na kusisitiza kuwa akina mama wawe mstari wa mbele Zaidi kusimamia na kufuatilia maendeleo ya elimu ya watoto wao.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amewakumbusha akina mama kufuatilia nyendo za watoto wao katika hiki ambacho dunia imebadilika na kuongeza kuwa ni jukumu na wajibu wa jamii nzima kumlinda mtoto bila kubagua ni mtoto wan ani.
Awali, akitoa salamu za wabunge wanawake wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Salma Kikwete Mbunge wa Jimbo la Mchinga amewaasa wanawake kuwapeleka watoto wao shule ikiwa ni njia mojawapo ya kujiandaa na ujio wa mradi mkubwa wa gesi asilia LNG ambao unaenda kutekelezwa katika Manispaa ya Lindi, Kijiji cha Likong’o.
Mhe. Salma amewaambia wanawake agenda ya elimu ni agenda muhimu kwa ustawi wa mwanamke na mwanadamu kiujumla, hivyo amewasisitiza kutumia vyema fursa ya elimu bure na miundombinu ya shule bora inayojengwa na serikali ya awamu ya sita kwa kuwapeleka shule watoto wao na kusimamia maendeleo yao ya kielimu.
Jenipher Valentino Sungu, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Nangano iliyopo wilaya ya Liwale amewasihi wanafunzi hasa wasichana kutumia vyema teknolojia zilizopo ikiwemo matumizi bora ya simu janja za mkononi na kompyuta kwa kukuza uelewa na kuboresha maarifa na kuepuka matumizi yanayoharibu maendeleo na tamaduni kwa ujumla.
Kila mwaka, ifikapo Machi 08, dunia huadhimisha Siku ya Mwanamke ambayo huwakutanisha wanawake kutoka maeneo tofauti kwa lengo la kubadilishana na kujengeana uwezo katika ushiriki wa maendeleo yao, jamii na taifa kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.