Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab R. Telack amewataka wanawake wote ndani ya mkoa wa Lindi kujikita zaidi katika shughuli za kilimo na kuongeza kipato katika familia zao na kujipatia uhakika wa uwepo wa chakula katika familia ili kupunguza magonjwa yatokanayo na lishe duni kwa watoto.
Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo katika sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika wilaya ya Ruangwa ambapo pia amewataka wanawake kutambua kuwa ndio msingi mkubwa kwa ustawi na maendeleo ya familia.
“Mtoto akiumwa utapiamlo ni mama ndiye anaekwenda nae hospitali na sio baba, wewe mwanamke ndio utakaeacha shughuli zako ili ubaki na mtoto hadi atakapokua sawa na ndio maana nasisitiza tuingie sasa katika shughuli za kilimo kwa mazao ya chakula ili tuhakikishe vyakula havipotei majumbani mwetu na watoto wetu hawakai na njaa, hii itawasaidia hata katika kujifunza kwao wawapo mashuleni” Mhe. Telack.
Mbunge wa jimbo la Mchinga Mhe. Mama Salma Kikwete amewataka Wanawake kujivunia mafanikio waliyoyapata katika Nyanja mbalimbali hasa za uongozi ambapo amesema “Leo hii tupo hapa tunafurahia matokeo na mafanikio yetu tukiwa na raisi mwanamke Mhe. Samia Suluhu, tuna spika wa Bunge mwanamke Mhe. Tulia Ackson, na hapa Lindi tumeletewa Mkuu wa Mkoa mwanamke Mhe. Telack ambaye ni mchapakazi na jasiri, hakika hatuwezi kushindwa na kitu.
Aidha, katika maadhimisho hayo wanawake wametakiwa kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia katika ngazi za mitaa na kushirikiana ili kuwawezesha wanawake wenye sifa za kua viongozi wanashika nafasi hizo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.