Watanzania watakiwa kutunza na kulinda tamaduni zao
Mhe. Kassim Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani amewataka watanzania kutunza na kulinda tamaduni zao kwa maendeleo ya taifa.
Haya aliyasema alipotembelea tamasha la utamaduni wa watu wa mkoa wa Lindi lililofanyika katika kijiji cha makumbusho ya taifa mkoani Dar es Salaam kuanzia tarehe 25-28/10/2018. Katika tamasha hili wanalindi walipata fursa ya kuonyesha mambo mbalimbali yanayohusu tamaduni zao mfano, ngoma, vyakula, vifaa vya jadi, nyumba zao, ikiwa ni pamoja na uwasilishaji wa mada mbalimbali zinazohusu tamaduni na maendeleo ya mkoa kwa ujumla.
Mhe. Majaliwa alisema kuwa kupitia matamasha kama haya watanzani wanapata fusa ya kujifunza tamaduni za watu wa mikoa mingine na hii inasaidia kuendelea kuwafanya watanzania kuwa na mshikamano. Pia aliwasihi wanalindi kuhakikisha wanalitumia vizuri tamasha hilo kwa kuonyesha tamaduni zao na kutangaza fursa mbalimbali zilizopo katika mkoa ili wawekezaji waweze kuja kuwekeza.
“Serikali itaendelea kulinda na kutunza tamaduni za watanzania kwa maendeleo ya taifa”, alisema Mhe. Majaliwa. “Serikali inatambua umuhimu wa tamaduni zetu katika kusimamia maadili ya watanzani na hivyo kusaidia kuwa na taifa la wananchi wenye maadili hasa kwa kundi la vijana ambalo kwa sasa limeonekana kuporomoka kimaadili”, aliongeza Mhe. Majaliwa.
Aidha, amewapongeza wanalindi kwa kujitokeza kwa wingi kuja kushiriki katika tamasha na ameipongeza kamati kwa ujumla ikiongozwa na Mhe. Godfrey Zambi, Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwa kazi kubwa na nzuri ya maandalizi waliyoifanya.
Pia aliuagiza mkoa kwa kushirikiana na kijiji cha makumbusho kuangalia uwezekano wa tamasha hili liwe linafanyika kila mwaka tarehe 25-28 October. Vilevile mkoa umeagizwa kutafuta eneo ambalo litakuwa ni katikati kwa wilaya zote na kuanza taratibu za ujenzi wa makumbusho katika mkoa ambapo vitu mbalimbali vya tamaduni za watu wa mkoa wa Lindi zitaonyeshwa na matamasha ya utamaduni ndani ya mkoa yatakuwa yakifanyika hapo.
Naye Mhe. Zambi alimshukuri Waziri Mkuu kwa kuja kutembelea tamasha na kujionea mambo mbalimbali ya tamaduni za watu wa Lindi ambapo pia alimuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote aliyoyatoa. Pia aliwapongeza makumbusho ya taifa kwa ushirikiano mkubwa walioutoa wakati wa maandalizi ya tamasha hili pamoja na kamati ya maandalizi.
Mkurugenzi wa kijiji cha makumbusho, Bi. Agnes Pinda alisema kuwa katika tamasha hili wanajamii wa mkoa wa Lindi wameshiriki vuzuri sana kwa kuonyesha mambo mbalimbali ya tamaduni zao. Vilevile wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam nao wamefika kwa wingi ikiwa ni pamoja na wageni kutoka nje ya nchi. Ni waombe wanalindi kuendelea kujitoa na kujitokeza kwa wingi pindi matamasha kama haya yanapoandaliwa.
Mmoja wa washiriki wa tamasha hili Bw. Kindamba amesema tamasha hili ni zuri sana kwani limewakutanisha wasaniii mbalimbali wa ngoma, na sanaa nyingine ambapo wanapata fursa ya kujifunza mambo mengine kupitia wenzao.
Aidha, Mhe. Majaliwa aliwapa salam za Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania washiriki wa tamasha na kuwaeleza kuwa anawapongeza wanalindi kwa kufanikisha tamasha hili.
Mhe. Majaliwa pia aliwaeleza kuwa kwa sasa serikali imesitisha minada ya korosho kutokana na kushuka kwa bei ili iweze kufanya tathmini ya kina na kutafuta ufumbuzi wa soko hilo. Hivyo amewasihi wakulima wa korosho kuwa watulivu katika kipindi hiki ambachoserikali inalifanyia kazi suala hili.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.