Watumishi watakao kwamisha zoezi la upigaji chapa mifugo kuchukuliwa hatua.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ameziagia halmashauri za mkoa wa Lindi kuhakikisha wanatekeleza agizo la upigaji chapa ng’ombe na watumishi watakao kwamisha zoezi hili watachukuliwa hatua.
Mhe. Ulega aliyasema hayo baada ya kukuta utekelezaji wa agizo la upigaji chapa mifugo upo chini huku halmashauri ya Kilwa ikiwa bado haijaanza kutekeleza. Mkoa wa Lindi una jumla ya ng’ombe 61,198 ambapo mpaka Mhe. Waziri anapita ng’ombe 8,545 walikuwa wameshapigwa chapa.
“Zoezi la upigaji chapa mifugo lipo kisheria na ni agizo alilolitoa Mhe. Rais hivyo kiongozi au mtumishi yoyote atakaye kwamisha utekelezaji wa agizo hili atachukuliwa hatua kali, hivyo niwatake viongozi na wataalam kuhakikisha kabla au ifikapo tarehe 31 January, 2018 zoezi hili liwe limekamilika”, alisema Mhe. Ulega.
Aidha, Mhe. Ulega aliwaagiza maafisa mifugo kwenda kwa wafugaji kutoa elimu ya ufugaji bora na matumizi ya mbegu bora zinazozalishwa katika kituo cha mbegu za uhamilishaji kilichopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa. Pia aliwaeleza maafisa mifugo kupitia upya takwimu za upigaji chapa na kuhakikisha takwimu sahihi zinapelekwa wizarani.
Katika ziara yake hii, Mhe. Ulega alikutana na wavuvi na wachuuzi wa samaki katika soko la samaki la manispaa ya Lindi ambapo aliuagiza uongozi wa Manispaa ya Lindi kuhakikisha wanatoza ushuru wa samaki kwa asilimia tatu badala ya tano wanazotoza sasa.
Pia aliwaagiza viongozi wa manispaa kufanya mazungumzo na mamlaka ya bandari ili kuwaomba sehemu ya eneo kwa ajili ya ujenzi wa soko ambapo soko lililopo sasa halifai na lilijengwa toka wakati wa mkoloni. Vilevile aliwashauri waendelee kuwashirikisha wavuvi katika maamuzi mbalimbali wanayofanya yanayowahusu.
Awali akitoa taarifa ya Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi alimueleza Waziri kuwa Mkoa wa Lindi unaendelea kupambana na uvuvi haramu licha ya changamoto zilizopo katika kupambana na wavuvi haramu zikiwepo za uhaba wa vifaa na fedha ambapo ameiomba wizara kuangalia uwezekano wa kusaidia hasa upatikanaji wa boti.
Vilevile Mhe. Zambi alisema kuwa mkoa unaendelea kutatua migogoro iliyopo kati ya wafugaji na wakulima na ile ya mipaka. Na kwamba mkoa utasimamia utekelezaji wa agizo la serikali la upigaji chapa mifugo kwa kuendelea kuwasimamia watendaji katika halmashauri.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.