Watumishi watakiwa kufanya kazi kwa kujituma
Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Bi. Rehema Madenge amewataka watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa kufanya kazi kwa kujituma na kuhakikisha wanatoa huduma bora.
Bi. Madenge aliyasema hayo wakati alipofanya kikao na watumishi hao kilichojadili masuala mbalimbali ya kiutendaji, na kiutumishi kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi na utoaji huduma bora kwa wateja. Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa.
Watumishi wametakiwa kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea badala yake wafanye kazi kwa kujituma na kujitolea ili wateja wa ndani na nje ya ofisi waweze kupata huduma bora.
“Sote tunapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, uadilifu, upendo, kuheshimiana na ushirikiano”, alisema Bi. Madenge. ‘Watumishi mnapaswa kuheshimiana licha ya kuwa na cheo kama zilivyo mila na desturi za watanzania’, aliongeza Bi. Madenge.
Aidha, watumishi wametakiwa kufuata miongozo mbalimbali ya kiutendaji inayotolewa ili kujiepusha na matatizo yanayoweza kuwapata kutokana na kutoifuata. Pia amewashukuru watumishi kwa mapokezi mazuri na ushirikiano waliompa tangu alipofika mkoa wa Lindi huku akiwasihi kuendelea na ushirikiano huo kwani ndio njia kubwa itakayoweza kuleta mafanikio.
Naye Katibu Tawala Msaidizi – Utawala na Utumishi, Dkt. Bora Haule alisema kuwa sehemu yake inaendelea kufanya maboresho kwa kuhakikisha stahiki za watumishi zinasimamiwa kwa mujibu wa taratibu na miongozo inayotolewa. Pia aliwasihi watumishi kuendelea kutoa taarifa pale wanapoona kuna tatizo ili waweze kupatiwa huduma kwa wakati.
Lucas Mbembela, Mchumi kutoka sehemu ya Serikali za Mitaa alisema kikao hicho kimetoa fursa kwa watumishi kujadili mambo mbalimbali zikiwemo changamoto wanazokutana nazo hivyo ni imani yake kuwa yale yote yaliyojadiliwa yatafanyiwa kazi.
Hawa Hatibu alisema kikao kama hicho kinasaidia kujadili mambo muhimu ya taasisi na kutoa fursa kwa watumishi katika ngazi zote kuweza kutoa malalamiko, maoni au ushauri lengo likiwa ni kuimarisha utoaji bora wa huduma kwa wateja wa ndani nan je.
Kikao cha watumishi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Lindi kimejadili mambo mbalimbali kiutendaji na kiutumishi kwa lengo la kuimarisha masuala ya kiutendaji na maslai ya watumishi lengo likiwa ni kuona namna ya kufanya maboresho katika utendaji na utoaji huduma kwenye mwaka huu mpya wa fedha 2019/2020.
PICHA MBALIMBALI ZA WATUMISHI WAKIWA KATIKA KIKAO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.