Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab R. Telack amewataka wazazi na walezi wa wanafunzi ndani ya mkoa wa Lindi kushirikiana na walimu katika kuhakikisha maendeleo ya kitaaluma na kinidhamu kwa wanafunzi na kubainisha kuwa ushirikiano huo utapunguza mzigo kwa walimu kitaaluma na kumfanya mzazi apate tathmini ya kile anachojifunza mtoto wake awapo shuleni.
Mhe. Telack ameyasema hayo katika hafla ya utoaji wa tuzo za kielimu iliyofanyika katika wilaya ya Kilwa, iliyoratibiwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Lindi na kuhudhuriwa na watumishi mbalimbali kuanzia ngazi ya Halmashauri, viongozi wa chama na serikali, walimu wa shule mbalimbali za umma na binafsi pamoja na wanafunzi.
“Wazazi wawafuatilie watoto wao na kutoa ushirikiano mzuri kwa walimu ili kupunguza mzigo katika malezi ya wanafunzi hawa wawapo katika mazingira ya shule, lakini pia mwanafunzi ana wajibu wa kusoma kwa bidii na kufanya tathimini ili kujua kile ambacho amejifunza darasani akiwa na mwalimu amekielewa kwa kiasi gani’’ amesema Mhe. Telack.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ametoa pongezi kwa watumishi wote kuanzia ngazi za wilaya, halmashauri, walimu na wanafunzi kwa kazi nzuri iliyofanywa na kupelekea mkoa kushika nafasi ya 8 kitaifa kutoka nafasi ya 26 na kubaki katika nafasi ya kwanza kati ya mikoa miotatu iliyopandisha ufaulu wa wanafunzi kwa miaka mitatu mfululizo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Zainab R. Kawawa amewataka wanafunzi kutunza mazingira na miundombinu wanayoitumia kujifunzia ili iweze kuwanufaisha na wanafunzi wengine pale kipindi chao cha masomo kitakapo hitimika.
“Niwaombe wanafunzi muongeze bidii katika kujifunza, muongeze juhudi katika kuhudhuria masomo yenu na pia kutunza miundombinu yenu ya kujifunzia ikiwemo majengo, madawati na vitabu pia ili mkimaliza nyinyi vije viwanufaishe na wengine” amesema Mhe. Kawawa.
Hafla hiyo ilihusisha utoaji wa tuzo, vyeti vya pongezi na zawadi za pesa taslimu kwa halmashauri, walimu na wanafunzi walioibuka vinara katika matokeo ya kitaifa kwa lengo la kupongezana na kupeana motisha ya kuendelea kufanya vizuri zaidi ambapo pia zoezi hilo lilipambwa na burudani mbalimbali za mashairi, ngonjera, ngoma na nyimbo mbalimbali zilizoandaliwa na walimu pamoja na wanafunzi mbalimbali wa shule za msingi na sekondari.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.