Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt Seleman Jafo (Mb) amekagua ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Mpilipili iliyopo Manispaa ya Lindi, wilaya ya Lindi wakati wa ziara Maalumu ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye kauli mbiu 'Rais Samia na Maendeleo, Wasikie na Waone'.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Nachingwea baada ya kukagua ujenzi wa jengo la bweni hilo, Waziri Jafo amewataka wazazi wa watoto wenye mahitaji maalum kutumia fursa hiyo ili watoto wao wapate elimu kwa kuzingatia kwamba nao wana haki sawa kama watoto wengine ya kupata elimu.
" Mhe. Rais anajipambanua sana kuhakikisha watoto wote na wazazi wananufaika na upatikanaji wa huduma za elimu bure kuanzia ngazi za awali hadi sekondari bila ubaguzi hivyo niwaombe wazazi ambao wana watoto wenye mahitaji maalumu wasiwafiche watoto wao, waone fursa hii na wawalete watoto wao shuleni ili wapate elimu" Mhe. Jafo.
Aidha, Mhe.Jafo ameeleza kuwa ni dhamira ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuwa watanzania wote na wanaLindi kwa ujumla wananufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo uboreshaji wa huduma za afya ambapo kwa Mkoa wa Lindi pekee hospitali mpya nne za wilaya zimejengwa, ukarabati wa hospitali ya Kinyonga iliyopo Kilwa Kivinje iliyogharimu kiasi cha Tsh. Milioni 900, ujenzi wa vituo vya afya katika maeneo mbalimbali, zahanati pamoja na magari ya kubebea wagonjwa (ambulance) 13 ambapo wakazi wa manispaa ya Lindi wamenufaika kwa kupatiwa magari hayo mawili.
"Viongozi wa chama na serikali pamoja na wananchi Mhe. Rais anafanya uwekezaji wa fedha kwenye miradi ya sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu, Kilimo, Uvuvi na Miundombinu sasa ni wajibu wenu kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na matumizi ya fedha zilizoletwa na serikali ili iweze kukamilika kwa wakati uliopangwa, kikamilifu na kuleta matokeo yenye tija kwa mustakabali wa kunufaisha na kuboresha maisha ya wananchi" Mhe. Jafo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.