Mheshimiwa Zainab Telack, Mkuu wa mkoa wa Lindi amewataka wazazi kuacha tabia ya kukaribisha wageni majumbani na kuwaruhusu kulala na watoto wao ili kuzuia matukio ya ukatili kwa watoto ikiwemo ubakaji na ulawiti.
Mkuu wa mkoa ameyasema hayo wakati wa Maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika yanayofanyika June 16 kila mwaka, ambapo katika mkoa wa Lindi maadhimisho hayo yamefanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu (TTC) wilayani Nachingwea.
“Wazazi acheni kukaribisha wageni na kuwaruhusu walale chumba kimoja na watoto wenu, baadhi yao hapo ndio hupata mwanya wa kuwafanyia vitendo vya unyanyasaji watoto kama ubakaji, kisha huwatishia kuwaua kama ikitokea kusema na kwakuwa hata sisi wazazi huwaamini sana wageni kuliko watoto ndio hushindwa kabisa kusema kinachowapata, niwaambieni watoto toeni taarifa yoyote ya ukatili kwa mtu aliyekuzidi umri, unayemwamini na mwenye busara” Mkuu wa mkoa.
Vilevile,Mkuu wa Mkoa amewataka wazazi kutambua kuwa familia ndio msingi mkuu wa kwanza katika malezi ya mtoto hivyo ni wajibu wa wazazi kumlinda, kumjenga na kumsimamia mtoto aishi kwa amani na upendo, aweze kuwa na maendeleo mazuri shuleni ili atimize malengo yake , na kubainisha kuwa hayo yatawezekana kwa kupunguza migogoro ndani ya familia kwani kwa kiasi kikubwa huchochea unyanyasaji wa watoto na kuongezeka kwa watoto wa mitaani.
Awali akisoma risala, Nasra Liegwa Mwakilishi wa Baraza la watoto Mkoa wa Lindi, ameiomba serikali kuimarisha huduma za afya kwa watoto kuanzia miundombinu ya kujifungulia kwa wamama wajawazito, huduma za kliniki ikiwemo chanjo na kuhakikisha uwepo wa huduma za kwanza mashuleni kwa ajiri ya huduma za awali.
”Jamii inapaswa kuweka mazingira sahihi ya ulinzi kwa watoto kwa kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya mtoto wa mwenzio ni kama mtoto wako, kwa kuboresha ulinzi katika maeneo kama kilabu za pombe na madisko kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anahudhuria katika maeneo hayo, aidha viongozi wa dini kutoa semina za mafundisho ya ndoa na ujenzi wa familia bora ili kuepusha migogoro na uvunjifu wa familia” ameongeza.
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka 2022, yamekuwa na kauli mbiu isemayo “Tuimarishe Ulinzi kwa Mtoto, Tokomeza ukatili dhidi yake, Tujiandae Kuhesabiwa”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.