Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt Seleman Jafo ametembelea mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa juhudi za serikali za kuimarisha miundombinu ya sekta ya uvuvi nchini.
Ziara hiyo imekuja wakati utekelezaji wa ujenzi wa bandari hiyo ukiwa kwenye hatua muhimu, huku mradi huo ukitarajiwa kuleta mafanikio makubwa kwa wavuvi, jamii ya Kilwa na taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri Jafo ameeleza kuwa ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na kusisitiza kuhusu dhamira ya serikali ya awamu ya sita ya kuwekeza na kuboresha miundombinu muhimu ambayo itasaidia kukuza sekta ya uvuvi na biashara zinazohusiana na rasilimali bahari.
"Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa ni sehemu ya mpango mpana wa serikali wa kuboresha miundombinu ya kiuchumi, tukumbuke kuwa katika nchi, huu ni uwekezaji wa kwanza mkubwa katika bandari hii kubwa nzuri ya uvuvi ambayo itabadilisha kabisa uchumi wa taifa letu hili katika sekta ya uvuvi. Ndani ya muda mfupi tukumbuke Mhe. Rais ametoa Bil 266 kwa ajiri ya mradi huu na tunaona utekelezaji wake unakwenda vizuri." amesema Waziri Jafo.
Aidha, Mhe. Jafo ameongeza kuwa, bandari hiyo itasaidia kurahisisha shughuli za uvuvi huku ikifungua fursa za kibiashara kwa wananchi na kuongeza thamani ya mazao bahari hususan samaki, kufungua fursa za uwekezaji wa samaki kutokana na kusaidia upatikanaji wa malighafi kwa urahisi hivyo uchumi wa nchi kuendelea kujikita zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack ameishukuru serikali kwa uamuzi wa kuiwezesha Halmashauri ya Kilwa kuwa kitovu cha bandari ya kwanza ya uvuvi ya kisasa na kueleza kuwa fursa hiyo inakwenda kuwapatia wavuvi soko la uhakika la samaki wanaowavua pamoja na kuwawezesha wajasiriamali na wawekezaji kupata eneo maalumu la kupata malighafi.
Ziara ya Waziri wa Viwanda na Biashara katika ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa inaashiria hatua kubwa katika kuimarisha sekta ya uvuvi, ikifungua fursa za ajira na kuboresha maisha ya jamii ya wavuvi. Hii ni ishara ya uwekezaji endelevu wa serikali katika miundombinu na uchumi wa buluu kwa maendeleo ya taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.