Waziri Mkuu leo asubuhi katika ziara yake Wilayani Nachingwea, Mkoani Lindi ameonesha kusikitishwa kwa jeshi la Polisi kutochukua hatua dhini ya wahalifu.
Akizungumza na wafanyakazi wa hospitali ya Wilaya ya Nachingwea alipofika hospitalini hapo kukagua ujenzi jengo la wodi ya hospitali hiyo, Mhe. Majaliwa amehoji jeshi la polisi toka mwezi wa tisa kushindwa kuwachukulia hatua watendaji walioiba nondo za ujenzi wa mradi huo.
“Kama tunakuwa na watumishi wa umma wanawaibia wananchi, halafu tunasema tunapeleleza….haiwezekani.” amesema Mhe. Majaliwa.
Aidha, amelitaka jeshi la Polisi kuchukua hatua mara moja ili watumishi wa serikali watambue wajibu wao kwa kufanya kazi kwa uadilifu na kuwaletea wananchi wa Nachingwea maendeleo. Mhe. Majaliwa amemtaka Mganga Mkuu wa Wilaya, DMO kuwa makini katika usimamizi wa fedha za miradi kwani fedha nyingi zitaletwa Wilayani Nachingwea ikiwemo milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa ICU, milioni 90 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amemueleza Waziri Mkuu kuwa viongozi na watumishi wa Mikoa na Wilaya wapo tayari kusimamia fedha za miradi ya afya na elimu zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.