WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUPAMBANA NA UVUNAJI HARAMU WA MISITU.
Naibu waziri wa maliasili na utalii Mhe. Constantine Kanyasu amesema wizara yake imejipanga kupambana na uvunaji haramu wa misitu, hali inayosababisha jangwa na ukosefu wa maji nchini.
Hayo aliyasema wakati akijibu maswali aliyoulizwa katika banda la JKT wakati wa maonesho ya nanenane Kanda ya Kusini yaliyofanyika katika viwanja vya Ngongo – Manispaa ya Lindi.
Katika majibu yake naibu waziri amesema wizara inajitahidi kuzuia ukataji miti unaofanywa na wamiliki wa ardhi za vijiji na kuwakumbusha kuwa wanapaswa kushirikisha wizara husika pale wanapotaka kukata miti katika maeneo yao ya ardhi.
“Kwa maeneo yaliyopo chini ya uongozi wa kijiji, wamiliki wa mashamba ni lazima washirikishe wizara ya maliasili na utalii wanapotaka kukata miti ambapo wanahitajika kuandaa mpango wa upandaji miti katika eneo jingine pamoja na matumizi ya miti wanayoikata kwa sababu wengi wamekuwa wakikata miti na kuichoma wakati ingefaa kwa matumizi ya nishati katika kijiji kizima”, alisema Mhe. Kanyasu.
Waziri Kanyasu ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuelewa kuwa mashamba ni ya kwao lakini miti iliyopo ndani ya mashamba hayo ni ya serikali hivyo basi wanapaswa kutoa taarifa pale wanapohitaji kuikata. Aidha, ametoa rai kwa wakulima kuacha kilimo cha kuhamahama badala yake maafisa kilimo wawape elimu ya kilimo ili kutunza mazingira.
Wizara itasimamia wakulima hasa wa ufuta ambao huacha kutumia mashamba yao ya zamani na kuhamia katika maeneo mapya kuanza kufyeka misitu, na kuwapa elimu ya utaalamu wa magugu ili waweze kufanya shughuli zao bila kuhama katika maeneo yao.
Maonyesho ya wakulima nanenane mkoani Lindi yamekwenda sambamba na utoaji wa elimu mbalimbali kuhusu upandaji miti, utunzaji wa misitu na wanyamapori zilizotolewa na taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara ya maliasili na utalii kama TFS,TAWA na mamlaka ya uhifadhi wa msitu wa asili Rondo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.