Zambi atembelea ujenzi wa madarasa Lindi Sekondari.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi ametembelea shule ya sekondari ya Lindi kuona kazi ya ujenzi wa madarasa yaliyoungua kwa moto usiku wa kuamkia tarehe 10/07/2016.
Jengo la madarasa linalojengwa ni la gorofa tatu na linajengwa na SUMA JKT. Jengo hili litagharibu karibu bilioni mbili ambapo katika harambee iliyofanywa ikiongozwa na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) fedha na vifaa zilizopatikana zilikuwa zaidi ya milioni 500.
Mhe. Zambi ameridhishwa na kazi inayoendelea kufanyika ambapo amemkuta mkandarasi akiwa anaendelea na ujenzi wa msingi. Pia alipata maelezo ya namna kazi ya ujenzi wa msingi wa ghorofa itakavyoendelea kufanyika.
“Ujenzi huu ulichelewa kuanza kutokana na kukamilishwa kwa taratibu zikiwemo za kumpata mkandarasi na upimaji wa udongo. Lakini nashukuru sasa kazi imeanza na inakwenda vizuri”, alisema Mhe. Zambi. Aidha, amewaomba wadau na wananchi wote kwa ujumla kuendelea kuchangia fedha na vifaa ambavyo vitasaidia katika ujenzi wa jengo hilo. Vilevile amewaomba wale ambao walikuwa bado hawajakamilisha ahadi walizokuwa wametoa kukamilisha.
Naye Mkuu wa Shule ya Lindi Sekondari, Ndg. Tarimo alisema kuwa kazi ya ujenzi inakwenda vizuri japo zipo changamoto ndogo ambazo huwa zinafanyiwa kazi na viongozi. Pia ameeleza kuwa wanafunzi wanaendelea vizuri na masomo kwani vipo baadhi ya vyumba ambavyo wamelibadilisha matumizi kwa muda wakati wakisubiri jengo kukamilika. Vilevile amewaomba wananchi kuendelea kuchangia kwani kazi ya ujenzi bado ni kubwa.
Zambi pia aliwatembelea wanafunzi wa kidato cha pili ambao wanajiandaa kufanya mitihani ya kidato cha pili na kuwasihi wafanye maandalizi mazuri. “Wazazi wenu wamewaleta hapa shuleni kusoma hivyo mnatakiwa msome kwani elimu mtakayoipata hapa ni kwa faida yenu na si ya wazazi wenu” alisema Zambi.
Aidha, aliwataka wanafunzi kuwaheshima wazazi/walezi, walimu na jamii kwa ujumla. Vilevile aliwatakia masomo na mtihani mwema wa taifa wa kidato cha pili ambao utaanza kufayika tarehe 13 Novemba, 2017.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.