DC Nachingwea apewa maelekezo akiapishwa
Mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Hashim Abdallah Komba amepewa maelekezo 11 ya kwenda kuyafanyia kazi mara baada ya kuapishwa.
Maelekezo hayo yalitolewa na mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi baada ya kumuapisha mkuu huyo wa wilaya, tukio ambalo lilifanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa na kushuhudiwa na wakuu wa wilaya, kamati ya ulinzi ya mkoa, wakurugenzi wa halmashauri, viongozi wa dini na watumishi wa sekretarieti ya mkoa wa Lindi.
Zambi amemtaka mkuu huyo wa wilaya licha ya kutimiza majukumu yake kuhakikisha kwanza wilaya ya Nachingwea vizuri kwa haraka. Pia ahakikishe anaboresha mahusiano kati ya ofisi ya mkuu wa wilaya na ofisi ya mkurugenzi.
Maagizo mengine ni kusimamia ukamilishaji wa ukarabati wa soko ambalo lililalamikiwa na wananchi wakati wa ziara ya Rais Magufuli, kusimamia ujenzi wa mabweni Nachingwea high school, kuhakikisha mabasi yote yanahamia stand mpya na kuhakikisha miundombinu inaendelea kuboreshwa huku halmashauri ikitakiwa kulipangia matumizi eneo lililokuwa la stand ya zamani.
Pia amemtaka kutatua migogoro ya ardhi iliyopo ambapo aliutaja mgogoro wa viwanja katika eneo la Namatula, kusimamia utoaji wa vitambulisho vya wajasiriamali, kusimamia zoezi la usafi wa mazingira sambamba na ujenzi wa vyoo. Na kuhakikisha amani na utulivu inatawala katika kipindi chote cha kampeni na uchaguzi wa serikali za mitaa.
Vilevile Zambi amewaagiza wakuu wa wilaya kusimamia miradi ya ujenzi hasa katika miundombinu ya afya na elimu. Mkuu wa mkoa amewaagiza kusimamia matumizi ya POS kwa kujua idadi yake, ngapi zinazofanya kazi, mahitaji halisi katika halmashauri na nini kinafanyika ili kuhakikisha fedha zinakusanywa kwa kutumia mfumo. Katika hili mkuu wa mkoa Zambi amehitaji kupata taarifa kabla au ifikapo tarehe 30 Oktoba, 2019.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Mhe. Komba ameahidi kwenda kutimiza majukumu yake pamoja na maelekezo yote aliyopewa na mkuu wa mkoa. Pia amewaomba wananachingwea kumpa ushirikiano kwani kupitia ushirikiano ndio wataweza kukuza maendeleo ya Nachingwea.
Katibu Tawala Mkoa, Bi. Rehema Madenge aliwasihi viongozi na watumishi wote kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kama majukumu yao yanavyowataka ili kuhakikisha wanatoa huduma sahihi na kwa wakati kwa wananchi na kuhakikisha mkoa unasonga mbele kimaendeleo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.