Zambi awataka viongozi kuchukua hatua kuhusu tatizo la mimba za utotoni
Mkuu wa mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi amewataka viongozi kuchukua hatua kuhusu tatizo la mimba za utotoni linaloukabili mkoa.
Zambi ameyasema hayo katika kikao cha kujadili tatizo la mimba za utotoni kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa. Kwa taarifa za mpaka Novemba, 2019 mkoa ulikuwa na jumla ya mimba 151 ambapo kati ya hizo 43 ni za shule ya msingi huku 108 zikiwa ni za sekondari.
Idadi hii ya mimba ni kubwa na ndiyo iliyosababisha uongozi wa mkoa kuitisha kikao hicho, kwa lengo la kujadili ukubwa wa tatizo ili kuweza kutoka na mikakati itakayosaidia kupunduza kama sio kumaliza kabisa tatizo hilo.
Zambi amewataka viongozi katika ngazi zote kwenye mkoa kuhakikisha licha ya kuwachukulia hatua wale wote wanaohusika na tatizo hili, waunde kamati za ulinzi wa mtoto kwa kila wilaya ambazo zitakuwa na wajibu wa kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu madhara ya mimba za utotoni pamoja na mambo mengine.
Pia maafisa elimu na maafisa ustawi wa jamii wameagizwa kusimamia uanzishwaji wa klabu rika katika shule na kwa shule ambazo zipo, ziimarishwe ili kusaidia utoaji wa elimu rika kwa wanafunzi wa shule husika.
Wazazi nao wametakiwa kuwa wa kwanza kusimamia mienendo ya watoto wao kuanzia nyumbani, shuleni na katika jamii badala ya kuwaachia walimu na jamii ndio ifanye kazi hiyo kitu ambacho kina sababisha watoto wengi kukosa maadili.
Zambi amesema kutokana na kupungua kwa maadili ya watoto ni vema sasa viongozi katika kila ngazi kuhakikisha vipindi vya dini shuleni vinarejeshwa na kusimamiwa ufundishwaji wake. Aidha, halmashauri zimetakiwa kuweka mkakati wa kuhakikisha zinafanya upimaji wa mimba wa mara kwa mara kwa wanafunzi hasa wanapokuwa wanakwenda likizo na wanaporejea.
Wajumbe katika kikao hicho wameonyesha kutokuwa na imani na mambo yanayofundishwa kwenye jando na unyago hivyo wameamua kabla ya unyago watoto wanaopelekwa wote waandikishwe kwa watendaji wa vijiji na mitaa, msimamizi wa watoto hao afahamike ili kumuona kama anafaa kwenda kukaa na watoto na kujua ni mambo gani watoto wanakwenda kufundishwa na kufuatilia ufundishwaji wake ili kama kutakuwa na mambo yasiyofaa yaweze kuzuiwa.
Aidha, imeshauriwa kufanyika uchambuzi katika kila wilaya ili kujua ni maeneo gani ambayo yanaongoza kwa tatizo la mimba za utotoni na kuchukua hatua madhubuti kwenye eneo husika badala ya kubaki na taarifa za jumla za wilaya na mkoa.
Waluu wa wilaya wameagizwa kwenda kufanya kikao kama hiki ambacho kitawashirikisha wajumbe katika wilaya na maafisa tarafa nao wafanye katoka tarafa, lengo likiwa ni kushusha maazimio ya kikao hadi ngazi za chini.
Wajumbe kwa pamoja walikubaliana kufanya vikao hivi mara mbili kwa mwaka ambapo watafanya tathmini ya hali ya mimba za utotoni pamoja na mambo mengine yanayohusu watoto.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.