Zambi azuia uchimbaji wa dhahabu wilayani Nachingwea
Mkuu wa mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi amezuia uchimbaji wa dhahabu katika kijiji cha Mpiruka B wilayani Nachingwea.
Akitoa ufafanuzi wa hali ya eneo hilo, mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Hashim Komba alisema walibaini kuwa eneo hilo linachangamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vibali halali vya uchimbaji, wachimbaji kutokubaliana na mmiliki wa eneo hilo ambaye amelima mazao, kukosa vyoo, hakuna makusanyo yoyote ya serikali, na kulikuwa na ajira za watoto.
Lakini baada uongozi wa wilaya kuzungumza na wataalam wa madini walibaini kuwa eneo hilo lina leseni ya utafiti wa madini aina ya kinywe (graphite) ambayo illitolewa mwaka 2017. Wachimbaji wadogo wanalitumia eneo hilo kwa kuchimba dhahabu.
Kutokana na mapungufu hayo, mkuu wa mkoa Zambi aliwaeleza wachimbaji pamoja na wanakijiji kuwa amezuia uchimbaji huo kuanzia sasa mpaka hapo taratibu zinazotakiwa kufuatwa zitakapokamilishwa.
“Nauagiza uongozi wa wilaya uhakikishe unafunga shughuli zote za uchimbaji katika eneo hili mpaka hapo taratibu husika zitakapo kamilishwa” alisema Mhe. Zambi.
Aidha, mkuu wa mkoa Zambi amewataka wachimbaji wote ambao wametoka nje ya kijiji hicho kurudi kwao kwa kuwa kukamilika kwa taratibu hizo kutachukua muda wa zaidi ya miezi mitatu, na kwamba eneo hilo kwa sasa halitakiwi kufanyiwa uchimbaji kutokana na uwepo wa mazao yaliyopandwa na wamiliki hivyo ni lazima wasuburi kwanza mpaka wavune.
Pia ameuagiza uongozi wa wilaya kwa kushirikiana na kamishna wa madini kuhakikisha wanasimamia vizuri zoezi la fidia ili wananchi wanaomiliki maeneo hayo wapate haki yao. Hii ni pamoja na kuwasaidia wachimbaji hao wadogo na serikali ya kijiji kuweza kukamilisha taratibu zinazotakiwa ili shughuli za uchimbaji ziweze kuendelea hapo baadae.
Naye mmoja wa wamiliki wa maeneo hayo Bi. Zainabu Ng’ombo ameshukuru serikali kwa hatua zilizochukiliwa na viongozi za kusimamisha shughuli za uchimbaji. Bi. Ng’ombo amesema wachimbaji walikuta amepanda mazao yake kwa ajili ya chakula lakini walianza kuyang’oa wakati wakichimba madini na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa. Pia aliomba kama taratibu zitakamilika kwa wakati ni vema uthamini wa maeneo hayo ukafanyika ili wamiliki walipwe haki yao ambayo itawasaidia kuondokana na usumbufu wanaokutana nao.
Henrick Mustamba ambaye ni dereva bodaboda alisema uwepo wa wachimbaji hao ulikuwa ni fursa kwao kwani walikuwa wakiwabeba kila siku kuwapeleka machimbo kwa gharama y ash. 5,000. Pia walikuwa wakiuza maji kwenye madumu kitu ambacho kilikuwa kikiwaongezea kipato huku dumu moja la maji wakiuza kw ash. 1,500. Hivyo ameomba taratibu zinazohitajika kufanywa zifanyike kwa wakati ili shughuli hizo ziendelee.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.